Radio Fadhila
Radio Fadhila
21 March 2025, 10:05 AM

Mwananchi akipata huduma ya afya ya kinywa na meno katika viwanja vya Mashujaa, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara mkoani Mtwara. Picha na Godbless Lucius
Afya ya kinywa na meno ina uhusiano wa moja kwa moja na afya ya akili, kwani matatizo ya afya ya akili yanaweza kuathiri afya ya kinywa na meno.
Na Neema Nandonde
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Baraka Nzombo ameeleza kuwa kuwa akina mama wajawazito wenye changamoto za afya ya kinywa na meno, wanakabiliwa na hatari ikiwa ni pamoja na kifafa cha mimba, kujifungua watoto njiti, kupata watoto wenye uzito mdogo, au hata kupoteza ujauzito endapo hawapati matibabu mapema.
Amebainisha hayo Machi 20, 2025 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani, yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mashujaa, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara.

Maandamano ya amani yaliyobeba ujumbe kuhusu maadhimisho ya wiki ya afya ya kinywa na meno katika viwanja vya Mashujaa, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara mkoani Mtwara
Aidha, Dkt. Berege ameongeza kuwa afya ya kinywa na meno ina uhusiano wa moja kwa moja na afya ya akili, kwani matatizo ya afya ya akili yanaweza kuathiri afya ya kinywa na meno, na kinyume chake.
Amesema kuwa wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, wako kwenye hatari kubwa ya kupoteza kumbukumbu, kutokana na bakteria wa kinywa na meno kushambulia ubongo, hali inayoweza kusababisha matatizo ya afya ya akili.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amesisitiza kuwa afya ya kinywa na meno ni muhimu kwa ustawi wa afya ya akili, huku akiwataka wananchi kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha afya ya kinywa na meno, ili kuimarisha afya ya mwili kwa ujumla.
Maadhimisho hayo yametanguliwa na wiki ya huduma za matibabu ya meno, katika hospitali na vutuo vya afya ndani ya Halmashauri zote 9 za mkoa wa Mtwara, zikihusisha huduma za kuziba meno, kung’oa meno, kusafisha meno, upasuaji mkubwa na mdogo wa meno pamoja na kuweka meno bandia.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka 2025 ilikuwa “Kinywa chenye furaha, fikra tulivu”.