Radio Fadhila
Radio Fadhila
12 March 2025, 9:10 PM

Kitendo kinachoelezwa kama ‘kukataliwa’ kimesababishwa na ndugu wa marehemu kupewa maelekezo ya kwanza yasiyo sahihi, kutoka kwa mhudumu aliyewataka kwenda moja kwa moja kwenye geti dogo la kuingilia mochwari.
Na Neema Nandonde
Kufuatia mwanamke aliyejulikana kwa jina la Rukia Said, mkazi wa wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25-30, kukutwa na umauti ndani ya basi la abiria huku mashuhuda wakisema kuwa mwili wake ulikataliwa kuingizwa Mochwari, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine Dkt. Shadrack Msasi ametolea ufafanuzi suala hilo.
Tukio hilo limetokea Machi 11, 2025 ambapo marehemu huyo amefariki akiwa kwenye basi na alikuwa akisafirishwa kutoka Kilwa kuelekea Hospitali ya Rufaa mkoani Lindi – Sokoine kwa lengo la kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Mashuhuda, Mwili wa marehemu ulipofikishwa Hospitali, ulikataliwa kuingizwa ndani na kutelekezwa barabarani, huku ndugu wakiendelea kuomba msaada kutoka kwa wasamaria wema ili kurejea makwao kwa shughuli za mazishi.
Wameeleza kuwa sababu za kukataliwa kwa mwili huo, ni kukosekana kwa kitanda cha kubeba mwili na kuingizwa mochwari, jambo ambalo liliondosha matumaini ya kupatiwa huduma.
Akitolea Ufafanuzi, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani Lindi-Sokoine Dkt. Shadrack Msasi amekiri kutokea kwa sintofahamu hiyo, licha ya kukanusha kuwa, hospitalini hapo hawana utaratibu wa kakataa mwili kuingizwa ndani, bali kitendo kinachoelezwa kama ‘kukataliwa’ kimesababishwa na ndugu wa marehemu kupewa maelekezo ya kwanza yasiyo sahihi, kutoka kwa mhudumu aliyewataka kwenda moja kwa moja kwenye geti dogo la kuingilia Mochwari.
Baada ya maelekezo hayo, wakati basi hilo la abiria limeshashusha mwili na kuendelea na safari yake, baadae walipewa maelekezo ya kurejesha mwili huo geti kubwa, ili ufanyiwe vipimo kabla ya kupelekwa mochwari, jambo ambalo ndugu walikataa.
Amesema licha ya kutumia muda mrefu kuwashauri wapiti geti kubwa kwaajili ya uchunguzi zaidi, ndugu wao waliendelea kukataa na hatimaye wakakodi gari dogo na kuuweka mwili kwaajili ya kuusafirisha kuelekea nyumbani kwao.
Aidha, amekana taarifa ya kukosekana kwa vitanda katika Hospitali hiyo kama taarifa zilizovyotolewa na kuongeza kuwa, vifaa vyote vinapatikana na huduma zote za msingi zinatolewa kwa uhakika.
Mpaka mwili wa marehemu unaondolewa eneo la tukio bila ya, wasamaria wema wakiongozwa na jopo la madereva wa bodaboda Manispaa ya Lindi, walikusanya kiasi cha shilingi 101,100/= zilizokabidhiwa kwa ndugu pamoja na jeneza, ili kuhifadhi mwili wakati na baada ya kurejea makwao.