Radio Fadhila

Kamati ya siasa CCM yapongeza miradi Masasi Mji

7 March 2025, 12:01 PM

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Masasi Bi. Mariam Kasembe akiwa ameongozana na kamati ya siasa wakati wa ukaguzi wa miradi halmashauri ya mji Masasi. Picha na Godbless Lucius

Kamati hiyo imepongeza hatua ya halmashauri ya Mji Masasi, kwa kutumia mapato yake ya ndani katika mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi 2-1, katika kituo cha afya Mtandi uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 95.

Na Neema Nandonde

Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara,  imeridhishwa na kupongeza ubora wa miradi ya Afya na Elimu yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili,  inayotekelezwa Halmashauri ya Mji Masasi mkoani humo.

Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Masasi Bi. Mariam Kasembe akiongozana na wajumbe wa Kamati wametembelea na kukagua miradi hiyo Machi 6,2025 katika kata ya Marika, Napupa, Matawale, Temeke na Mtandi.

Kamati hiyo imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Amali Marika wenye thamani ya bilioni 1.6 inayojumuisha madarasa, ofisi, maabara, jengo la utawala, vyoo, jengo la maktaba, jengo la tehama, bwalo, kichomea taka na tanki la maji la ardhini.

Maeneo mengine ni mabweni ya wasichana na wavulana, nyumba ya mtumishi, karakana (automotive workshop) na viwanja vya michezo ambavyo ni vya mpira wa miguu, mpira wa pete na mpira wa wavu.

Aidha imetembelea zahanati ya Napupa, na kupongeza ubora wa zahanati hiyo iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 160.

Kamati hiyo pia imekagua na kupongeza hatua ya wanafunzi 146 kuanza shule katika shule Mpya ya Sekondari Matawale yenye thamani ya shilingi milioni 560 ambayo ina jengo la utawala, madarasa, maabara, maktaba, TEHAMA, matundu ya vyoo, kichomea taka, tanki la maji ardhi.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Masasi Bi. Mariam Kasembe akisalimiana na baadhi ya wajumbe wakati wa ukaguzi wa miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri ya mji Masasi. Picha na Godbless Lucius

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imepongeza hatua ya Halmashauri kutumia mapato yake ya ndani katika mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi 2-1, katika kituo cha afya Mtandi uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 95.