Mufindi FM

Wagombea CCM Mafinga wajipambanua kwa sera thabiti

2 August 2025, 11:51

Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini anayemaliza muda wake na mgombea anayetetea nafasi hiyo, Cosato David Chumi akinadi sera kwa wajumbe ili waendelea kumpa ridhaa ya kushirikiana naye katika kuleta maendeleo kwa wanamafinga, ikumbukwe kuwa Chumi ni miongoni mwa wagombea watano ndani ya CCM katika jimbo hilo. Picha na Isaka Nyigo.

Mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kwa nafasi ya ubunge Mafinga mjini unaonesha uimara wa demokrasia ya ndani ya chama hicho ambapo wagombea wanapata fursa ya kuwasilisha mawazo, sera, na dira zao moja kwa moja kwa wajumbe, ikiwa ni hatua muhimu inayotoa nafasi kwa wanachama kuchagua kiongozi anayewakilisha vyema .

Na Marko Msafiri

Katika kuelekea upigaji wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kumpata mgombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Mafinga Mjini, Wagombea mbalimbali wamejitokeza kujinadi mbele ya wajumbe wa chama hicho, huku wakipambanisha sera na maono yao kwa ajili ya kuleta maendeleo ndani ya jimbo hilo.

Wagombea wa nafasi hiyo ya Ubunge katika jimbo hilo, wamekutana na wajumbe wa Kata ya Boma, Kata ya Upendo na Kata ya Wambi, ambapo Mratibu wa Kampeni za ubunge kura za maoni (CCM) Maines Kiwelu ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Mufindi amewasihi wajumbe kutafakari kwa makini sera zilizotolewa na wagombea katika kufanya maamuzi na kuwataka waache makundi.

Sauti Maines Kiwelu Mratibu wa Kampeni za ubunge kura za maoni (CCM)

Akizungumza katika nyakati tofauti na wajumbe wa kata ya Boma na Upendo, mbunge anayemeliza muda wake (anayetetea) nafasi hiyo ya ubunge ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato David Chumi ameeleza mafanikio na dhamira yake ya dhati ya kuendelea kushirikiana na wana Mafinga katika nafasi hiyo, akiweka wazi dhana yake ya ‘kazi zinaongea’.

Sauti Cosato Chumi

Mgombea mwingine wa nafasi hiyo ya ubunge ndani ya CCM ni Agrey Tonga ambaye amewaahidi mapinduzi ya maendeleo iwapo watampa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho.

Sauti Agrey Tonga.

Wengine ni Dickson Nathan Lutevele, Mendrad Kigola na Dkt. Bazil Lwisijo Tweve wameomba ridhaa kwa wajumbe huku wakieleza vipaumbele mbalimbali iwapo wakiaminiwa.

Sauti Dickson Lutevele & Dkt. Bazil Tweve

Wagombea hao baada ya kuhitimisha kunadi sera zao, kila mmoja amepata nafasi ya kuomba kura kwa wajumbe na kuwasihi wafanye maamuzi sahihi kwa mustakabali wa maendeleo kwa miaka mitano ijayo.

Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Boma iliyopo Jimbo la mji wa Mafinga wakiwasikiliza wagombea wa nafasi ya ubunge wa jimbo hilo katika viwanja vya ofisi za CCM wilaya zilizopo njini Mafinga.Picha na Isaka Nyigo

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM kuhusu michakato ya kuwapata wawakilishi watakaopeperusha bendera ya nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu, ambapo agosti 04, mwaka huu, wajumbe wa chama hicho watapiga kura za maoni ili kumpata muwakilishi katika nafasi hiyo ya ubunge.