Mufindi FM

Wafanyabiashara Mashujaa wagusa mioyo Isupilo, Makalala

14 July 2025, 12:25

Wafanyabiashara wa soko la Mashujaa mjini Mafinga katika picha ya pamoja na maafisa wa Jeshi la Magereza katika gereza la wafungwa Isupilo, wakikabidhi misaada kwa ajili ya kuwafariji wafungwa hao walipoenda kuwatembelea. Picha na Marko Msafiri.

Kujitoa kwa jamii ni kitendo cha kiugwana kinachoonyesha upevu wa kimaadili na upendo wa kweli. Ni tendo ambalo lina nguvu ya kubadilisha maisha ya watu, kuvunja mnyororo wa mateso na kuleta tumaini mahali palipojaa giza.

Na Marko Msafiri

Katika kuadhimisha dhana ya upendo kwa vitendo na kuonesha mshikamano na jamii yenye uhitaji, Wafanyabiashara wa soko la Mashujaa Mjini Mafinga wameonesha moyo wa huruma kwa kutembelea Gereza la wafungwa Isupilo na Kituo cha kulelea Watoto yatima cha Makalala kilichopo Mjini hapo.

Wakiwa na nia ya kugusa maisha ya watu walioko pembezoni mwa jamii, Wafanyabiashara hao wamefanya ziara maalumu katika maeneo hayo mawiliambapo wametoa misaada iliyogharimu kiasi cha Tsh Mil mbili (2) mavazi, sukari, sabuni na mahitaji mengine muhimu ya kila siku.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa soko hilo, Bw. Devick Kihindo amesema wameguswa na hali ya maisha ya watu walioko gerezani na Watoto yatima na kwamba jamii inayoendelea inapaswa kuwa na moyo wa kujitoa kusaidia wanyonge.

Bw. Kihindo ameongeza kuwa, kama wafanyabiashara wameshapanga mikakati ya kuendelea kufanya matendo hayo ya huruma, na kwamba kila baada ya miezi mitatu watakuwa wanawatembelea wahitaji mbalimbali.

Sauti Kihindo Mwenyekiti wa soko

Katika Gereza la Wafungwa Isupilo misaada hiyo, imepokelewa na Inspekta Faustin Mangula kutoka Ofisi ya Utawala ya Gereza hilo kwa niaba ya Mkuu wa Gereza hilo, ambaye amewashukuru Wafanyabiashara katika kutekeleza adhima yao ya upendo kwa vitendo.

Sauti Inspekta Faustin Mangula

Kwa upande wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Makalala, Kaimu Mkuu wa Makao hayo Philipo Kamoga amesema kituo kimejengwa kupokea watoto wachanga 35 lakini kwa sasa wana watoto 16 wanaowaleo huku 14 wakiwa shule na wawili wako katika makao hayo.

Sauti Philipo Kaimu Mkuu Makao Makalala

Baada ya kikabidhiwa misaada hiyo, kwa niaba ya wafungwa wa gereza la Isupilo, mmoja wa wafungwa wa gereza hilo, wameoneshwa kufurahishwa na kufarijika sana kwa kutembelewa na kujitoa kwao.

Sauti mwakilishi wa wafungwa

Msaada huo umepokelewa kwa furaha na shukurani kubwa kutoka kwa walengwa, na umeacha ujumbe wa wazi kuwa mshikamano wa kijamii hauhitaji utajiri mkubwa, bali moyo wa kujitoa.