Mufindi FM
Mufindi FM
14 July 2025, 11:59

Hapo awali wazalishaji wa mbegu walikumbana na changamoto mbalimbali zikwemo ukosefu wa elimu ya kiufundi, kutokuwa na uthibitisho rasmi, usambazaji holela na kukosa kuelewa mahitaji ya wakulima.
Na Marko Msafiri
Wakala wa Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) umeuhakikishia umma wa wakulima kuhusu mbegu zinazozalishwa kuwa ni bora na kwamba bidhaa hizo za mbegu zitakuwa na nembo ya TOSCI ili kumuepusha mkulima dhidi ya wazalishaji wasiokuwa na utaalamu au kuthibitishwa na taasisi hiyo.
Hayo yamejiri katika ukumbi wa Kangesa uliopo mjini Mafinga mkoani Iringa wakati wa utoaji wa mafunzo maalumu kwa wadau wanaojihusisha na uzalishaji wa miche ya miti na Matunda kwa lengo ikiwa ni kuwataka wazingatie ubora wa mbegu na miche ya miti katika viwango kwa mujibu wa taratibu na kanuni za mbegu husika.
Akizungumza Mkaguzi wa taasisi hiyo ya Udhibiti wa mbegu Tanzania anayehudunia Kanda ya Nyanda za juu kusini inayojumuisha mikoa saba (7) Bw. Meshaki Mhesi amesema lengo la mafunzo ni kuongeza ujuzi wa kuzalisha mbegu na miche ya uhakika na kwamba wanakuwa na uelewa wa kutambua kuwa wakulima wanahitaji kitu gani.
Sauti Mkaguzi kutoka TOSCI
Kwa upande wake Mtafti wa matunda kutoka Taasisi ya Utafti wa Kilimo (TARI) Bw. Daud Mbongo ametoa wito kwa wakulima kununua mbegu au miche ya matunda bora kutoka kwa wazalishaji wanaofahamika na waliopewa mafunzo kwani hao wanazalisha kwa kufuata miongozi na kanuni za mbegu husika.
Sauti Mtafti wa Matunda TARI
Nao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Dkt. Jerry Mduma ambaye ni mkulima wa parachichi kutoka Wilaya ya Kilolo ameongeza kwa kuwapongeza TOSCI kwa kuratibu mafunzo hayo yenye tija katika mnyororo wa thamani na kuiomba serikali idhibiti matumizi holla ya viuatilifu ili kuendelea kukidhi viwango vya kimataifa.
Sauti mshiriki Dkt.. Mduma
Jukumu kuu la taasisi hiyo ni kusimamia sheria ya mbegu namba 18 ya mwaka 2003 na kanuni zake ambazo zinatoa miongozo ya ugunduzi, uzalishaji na usambazaji wa mbegu kupitia kurugenzi mbalimbali za taasisi hiyo ikiwemo taasisi ya kuhakiki mbegu mpya (DUS) na umahiri wa mbegu nchini (NPT).