Wawili miaka 30 jela kwa unyang’anyi wa kutumia silaha
24 October 2024, 19:01
Na Bestina Nyangaro
Mufindi
Mahakama ya Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa imewahukumu Rashidi Mfikwa (34) na mwenzake Hussein Mfikwa(30) kifungo cha miaka 30 jela, kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya unyanganyi wa kutumia silaha.
Rashidi na husseni,wakazi wa kijiji cha Matanana kata ya Bumilayinga wilaya ya Mufindi Mkoani hapa, walikuwa wanakabiliwa na shtaka moja la unyanganyi wa kutumia silaha ambalo ni kinyume na kifungu namba 285 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Kesi hiyo ya jinai namba 22099 la mwaka 2024 ilikuwa na mashahidi 7 ambapo Hukumu yake imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Benedict Nkomola.
Akisoma hukumu hiyo Nkomola amesema kuwa ilielezwa mahakamani hapo kuwa mnamo june 4,2024 washtakiwa hao wakiwa na rungu walimvamia Mbaga majira ya saa 3 usiku wakati anajaribu kufungua geti la nyumbani kwake akiwa na mke na mtoto wake baada ya kufunga biashara yao katika kitongoji cha Legeza kijiji kilichopo katika kijiji hicho.
Aidha hakimu huyo alisema kuwa wameshtakiwa kwa kifungu 287A cha sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 rejeo la mwaka 2022.
Awali akizungumza kwa niaba ya washtakiwa hao kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili Msomi Emmanuel Chengula aliomba mahakama iwapunguzie adhabu kutokana na wakosaji hao ni kosa lao la kwanza na umri wao kuwa ni mdogo.
Kwa upande wake, Mwendesha mashtaka wa Serikali wakali Simon Masinga aliomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa washtakiwa hao kutokana kwamba mshtakiwa wa kwanza anakumbukumbu za awali za kufanya makosa jinai huku mashtakiwa wa pili akiwa hana kumbukumbu zozote za makosa hayo.
Mwisho