Mufindi FM

Ahukumiwa miaka 30 jela kwa kumbaka binti wa miaka 13

3 September 2024, 13:46

Na Beatrice Kaitaba

Mufindi

Mahakama ya Wilaya ya Mufindi imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Frank Ignas Kahise mwenye umri wa miaka 20 baada ya kupatikana na hatia kwa kosa la ubakaji kwa binti mwenye umri wa miaka 13.

Kesi hiyo ya jinai namba 16918 ya mwaka 2024 mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha sheria namba 130 kifungu kidogo cha 1 na cha (2)(e) na kifungu cha 131(1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 rejeo la mwaka 2022.

Akisoma hukumu hiyo tar 21 Agosti 2024 katika Mahakama ya wilaya ya Mufindi, hakimu mfawidhi Benedict Nkomola, amesema kuwa Mtuhumiwa huyo amehukumiwa kosa la kumbaka binti wa miaka 13 katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Mtuhumiwa huyo alimsafirisha mhanga kutoka Dodoma kwa lengo la kumtafutuia kazi, na walipofika Mafinga wakaenda katika nyumba za kufikia wageni na kuchukua vyumba viwili kila mtu cha kwake, majira ya usiku mtuhumiwa alienda katika chumba alichokuwa amelala binti na kumgongea, binti huyo alipobaini kuwa ni sauti ya mtu aliekuwa ameongozana nae kutafuta kazi alifungua mlango na kisha kijana huyo kuingia na kuanza kumuingilia kimwili kwa nguvu .

Ilipofika asubuhi mtuhumiwa aliondoka na binti huyo kuelekea katika nyumba nyingine ya wageni, alipata chumba kisha kumuacha binti huyo ndani na kumuahidi kuwa anaenda kumnunulia nguo.
Baada ya mtuhumiwa kutoka chumbani humu muhudumu wa nyumba hiyo ya wageni alienda kumuuliza mhanga mazingira ya yeye kuwepo pale.

Kwakuwa muhudumu alikuwa anamfahamu mtuhumiwa huyo alichukua jukumu la kutoa taarifa kwa uongozi wa serikaliya mtaa kisha akakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa upande wa mashtaka ndipo ikamuhukumu kutumikia kifungo hicho chini ya kifungu namba 235 (1) CPA cha sheria ya mwenendo wa makossa ya jinai huku mhanga akiwa chini ya usimamizi wa ustawi wa jamii kwaajili ya taratibu zingine.