Mufindi FM

Rais Dkt. Mwinyi ateta na Rais Widodo wa Indonesia

3 September 2024, 08:07

Pichani ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein(kushoto) katika picha ya pamoja na Rais wa Indonesia, Mhe. Joko Widodo, jijini Bali. Picha na MFA

Na mwandishi wetu

Bali

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo tarehe 2 Septemba 2024 jijini Bali, Indonesia amefanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Joko Widodo kuhusu masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Indonesia.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika mara baada ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika pamoja na Mkutano wa Viongozi kujadili ubia wa Maendeleo, Viongozi hao wamekubaliana kuendelea kusimamia utekelezaji wa makubalino ya ushirikiano katika sekta mbalimbali ambayo tayari yamesainiwa kwa nyakati tofauti baina ya nchi hizi mbili ili kuziwezesha kunufaika na ushirikiano huo.

Akizungumza baada ya mazungumzo yao, Mhe. Rais Mwinyi amesema Mhe. Rais Widodo ameonesha umuhimu wa kuanza utekelezaji wa makubalino mbalimbali ambayo tayari yamefikiwa na kuahidi kuendelea kuzihimiza kampuni zaidi za Indonesia kuja kuwekeza Tanzania hususan katika maeneo ambayo Indonesia imepiga hatua ikiwemo uchimbaji mafuta na gesi, kilimo na usarifu wa mwani, utalii na bandari pamoja na Rais huyo kuzitaka kampuni ambazo zipo chini ya Serikali yake kushirikiana na Tanzania katika maeneo hayo.

“Nimefurahi Mhe. Rais Widodo ameonesha utayari wa kuendelea kuzihimiza kampuni zaidi za Indonesia kuja kuwekeza Tanzania Bara na Zanzibar hususan katika maeneo ambayo tumekuwa tukihamasisha uwekezaji yaani bandari, uchimbaji mafuta na gesi, kilimo na usarifu wa mwani na utalii. Sasa ushirikiano wetu utaondoka katika hatua ya kukubaliana tuingie katika hatua ya utekelezaji”, amesema Mhe. Rais Mwinyi.

Aidha, Mhe. Rais Mwinyi amekutana na Waziri wa Utalii wa Indonesia, Mhe. Sandiaga Uno ambapo katika mazungumzo yao, Mhe. Sandiaga ameahidi kutoa nafasi kwa vijana wa Zanzibar kwenda nchini Indonesia kupatiwa mafunzo ya ujuzi kwenye sekta ya utalii ili kuwawezesha kuajirika. Itakumbukwa kuwa Indonesia imepiga hatua kubwa katika sekta ya utalii na kwa takwimu zilizopo nchi hiyo inatembelewa na takribani watalii milioni 12 kwa mwaka.