Mufindi FM

Mapilya: Utafiti wa udumavu Iringa urudiwe

18 July 2024, 17:22

Afisa Elimu Sekondari halmashauri ya wilaya ya Mufindi Mwl. Daniel Mapilya wakati akizungumza kuhusu tathmini ya matokeo ya kidato cha 6 kwa mwaka 2024, kwenye studio za Mufindi FM. Picha na Jackson Machowa

Na Jackson Machowa

Kutokana na ongezeko la ufaulu wa wanafunzi mashuleni, Idara ya Elimu Sekondari Wilaya ya Mufindi imeiomba serikali na watafiti nchini kufanya mapitio ya hali ya udumavu wilayani hapa kwa kuwa inakinzana na hali halisi ya maendeleo ya watoto kwa sasa.

Hayo yamesemwa na mkuu wa Idara hiyo wilaya ya Mufindi Mwl.Daniel Mapilya wakati akizungumza na redio Mufindi fm kuhusu tathimini ya matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2024 ambapo wilaya Mufindi imefaulisha kwa asilimia mia moja.

Aidha Mwl. Mapilya ameongeza kuwa elimu ya mapambano dhidi ya udumavu imesaidia kuielimisha jamii na hivyo kuwezesha wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapatiwa lishe bora wawapo nyumbani na shuleni.

Akizungmzia kuhusu matokeo ya mitihani ya kidato cha sita, Mwalimu Mapilya amesema wilaya Mufindi imeendelea kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani hiyo kwa miaka miwili mfululizo kwa kuhakikisha wanafunzi wanafaulu kwa wastani wa daraja la kwanza hadi la tatu.

Pamoja na wilaya ya Mufindi na mkoa wa Iringa kwa ujumla kuendelea kufanya vizuri matokeo ya mitihani mbalimbali ya kitaifa bado tafiti zinautaja mkoa huu kuwa na kiwango cha juu cha udumavu unaofikia asilimia 56.9 ukiwa ndio mkoa kinara wa udumavu nchini.