RC Manyara aagiza wakurugenzi kusimamia miradi
15 March 2024, 11:14 pm
Sendiga amewataka wakurugenzi wa halmshauri za mkoa wa Manyara kusimamia miradi ya kimkakati.
Na Mzidalfa Zaid
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amewataka wakurugenzi wa halmshauri zote za mkoa wa Manyara kuhakikisha miradi yote ya kimkakati inatekelezwa kwa wakati kutokana na fedha nyingi zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Sendiga amesema hayo katika kikao cha 37 cha kamati ya ushauri ya mkoa wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika kipindi cha miaka mitatu ambapo amesema kila mkurugenzi ana wajibu wa kuhakikisha anasimamia miradi hiyo.
Kwa upande wake kaimu katibu tawala msaidizi mipango na uratibu ofisi ya mkuu wa mkoa wa Manyara Lusungu Mwilongo amesema kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 mkoa wa Manyara umepokea Bilioni 270 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maendeleo na umeweka mpango wa bajeti kwa mwaka 2024/25 utakoendeleza miradi ya kimaendeleo.
Aidha meneja wa Ruwasa mkoa wa Manyara Mhandisi Wolter Kilter amesema mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa 5 ambayo ipo kwenye mpango maalum wa serikali wa kupeleka huduma ya maji vijijini na mpango huo utakuwa na awamu mbili na kila awamu itahusisha visimwa 5 kwa kila halmashauri.