Silo atoa magunia 10 ya mahindi kwa waathirika Manyara
22 May 2024, 7:10 am
Wakazi 500 katika kata Magara wilayani Babati mkoai Manyara wamekosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kufunikwa na maji ya ziwa Manyara kutokana na ziwa hilo kufurika kutokana na mvua.
Na Emmy Peter
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Babati Vijijini Danieli Silo ametoa magunia 10 ya mahindi kwa zaidi ya wakazi 500 kutoka kaya 311 katika kata Magara wilayani Babati mkoani Manyara ambao nyumba zao zimefunikwa na maji ya ziwa Manyara kutokana na ziwa hilo kufurika kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Akiongea na FM Manyara Silo amesema alifika katika eneo hilo akiambatana na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Babati Vijijini akiwemo mkurugenzi Anna Mbogo pamoja na Wakuu wa Idara ili kujionea hali halisi na kufanya tathmini ya athari iliyotokea kwa wakazi ambao wamekosa makazi ya kuishi kwa kuwapelekea mahema pamoja na chakula.
Aidha Silo amesema hakuna madhara yoyote yaliyojitokeza kwa wakazi hao zaidi ya mazao ya chakula kyalichokuwa katika mashamba ambayo hayajavunwa na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari ya maji hayo na kama walivyotangaziwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu mvua zinazoendele kunyesha .
Kwa upande wake mkurugenzi wa Babati vijijini Anna Mbogo amewapa pole wakazi hao nakusema Halmashauri inafanya utaratibu kwa ambao wamekosa mahala pakuishi na kama kunagarama zozote watagharamia.