Ruangwa FM

wanafunzi wataka mazingira salama ya hedhi mashuleni

6 November 2026, 14:19

picha ni wanafunzi shule ya secondary Ruangwa.

Wanafunzi wa kike Nachingwea wataka mazingira salama ya kujisitiri wakati wa hedhi ili kuepuka kukosa masomo, wakisisitiza umuhimu wa vyoo safi, maji na upatikanaji wa vifaa salama vya hedhi mashuleni.

Loveness Daniel

Ruangwa Lindi.

Ukosefu wa mazingira rafiki ya kujisitiri, vifaa vya hedhi na vyoo safi mashuleni ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kumfanya mtoto wa kike kukosa masomo wakati wa hedhi, hali inayowafanya wanafunzi mbalimbali kuwataka walimu na walezi kuhakikisha wanawaandalia mazingira salama na elimu sahihi kuhusu afya ya hedhi.

Wakizungumza na Ruangwa FM Radio katika shule ya msingi Chingunduli iliyopo wilayani Nachingwea, wanafunzi hao wamesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa maeneo maalumu ya kujisitiri pamoja na upatikanaji wa vifaa salama vya hedhi ili kuwawezesha kuendelea na masomo bila hofu wala aibu.

Sauti ya wanafunzi.

Utafiti wa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF wa mwaka 2021, kuhusu afya na usafi wa hedhi kwa wanafunzi wa kike, umebaini kuwa asilimia 16.8 ya wanafunzi walikosa masomo wakati wa hedhi katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya utafiti, huku asilimia 42 ya waliokosa shule wakitaja ukosefu wa vifaa vya hedhi na asilimia 34 wakitaja kukosekana kwa vyumba maalumu vya kujisitiri.

Kwa upande wake, mwalimu wa Sayansi, Ufundishaji na Malezi ya Mtoto katika shule hiyo, Ahmad Fundi, amesema pamoja na elimu ya hedhi kujumuishwa katika mitaala ya elimu, mazingira yasiyoridhisha katika baadhi ya shule yanaendelea kuwa changamoto katika kuwawezesha wanafunzi kujisitiri kwa usalama.

Amesema walimu wanashirikiana na wazazi kuwapatia watoto elimu na vifaa vya kujisitiri, huku akisisitiza umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi wa kike kuendelea na masomo hata wanapokuwa katika siku zao za hedhi.

Sauti ya Mwalimu Ahmad Fundi.

Akizungumzia umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi, Mratibu wa Afya ya Uzazi wilayani Ruangwa, Dkt. Fabiola Nyaki, amesema ni muhimu wasichana kupewa elimu ya hedhi kabla hawajaanza kupata hedhi kwa mara ya kwanza ili kuwaondolea hofu, aibu na dhana potofu zinazoweza kuwaathiri.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutumia vifaa safi na salama wakati wa hedhi na kuwashauri wanafunzi wanaopata hedhi nyingi kupita kiasi, maumivu makali yasiyovumilika, kizunguzungu au kuzimia kufika hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.

Sauti ya Dr Fabiola Nyaki