Ruangwa FM
Ruangwa FM
29 September 2026, 17:23

Wanawake wanaofanya biashara katika masoko na maeneo ya stendi wilayani Ruangwa wameeleza kukabiliwa na vitendo vya ukatili, udhalilishaji na kudhulumiwa kipato. Wameiomba jamii na mamlaka husika kuimarisha usalama katika maeneo hayo, huku Jeshi la Polisi likiwataka waathirika kuripoti matukio ya ukatili mapema ili hatua zichukuliwe.
Na Loveness Daniel.
Wanawake wanaofanya biashara katika masoko na maeneo ya stendi wilayani Ruangwa wamelalamikia kukabiliwa na vitendo vya ukatili, udhalilishaji pamoja na kudhulumiwa kipato wanachokipata baada ya kufanya biashara.
Wakizungumza na Ruangwa FM, baadhi ya wafanyabiashara na mama ntilie wamesema licha ya masoko na stendi kuwa maeneo muhimu kwao kutafuta kipato, wakati mwingine hukutana na vitendo vinavyowafanya wasijisikie salama katika maeneo yao ya kazi.
Malalamiko hayo yanaungwa mkono na Mwenyekiti wa Soko Jipya wilayani Ruangwa, ambaye amesema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara, hususani wanawake, kuhusu kudhulumiwa na kukabiliwa na vitendo vya ukatili.
Amesema pale malalamiko yanapowasilishwa, uongozi huchukua hatua zinazohitajika kwa lengo la kutafuta suluhisho na kuhakikisha mazingira ya soko yanakuwa salama kwa wafanyabiashara.
Katika jitihada za kupinga ukatili wa kijinsia katika maeneo hayo, baadhi ya wanaume wameeleza kuwa wanaume wenzao wana nafasi ya kushiriki katika kuzuia ukatili dhidi ya wanawake, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na kuwasaidia wanawake wanaokumbana na vitendo hivyo.
Afisa Polisi kutoka Kitengo cha Dawati la Jinsia, wilayani hapa Sajenti Happiness Lyatuu, amesema baadhi ya wanawake wanaokumbana na ukatili huishia kumalizana wenyewe bila kufikisha taarifa katika dawati hilo, jambo linaloweza kufanya matukio hayo kutotambulika rasmi,Amewahimiza wanawake wanaokumbana na ukatili kuripoti mapema ili waweze kupata msaada na hatua stahiki kuchukuliwa dhidi ya vitendo hivyo.