Ruangwa FM

Wananchi Ruangwa Watakiwa Kuendeleza Viwanja vyao kuepuka Hasara za kiuchumi

23 June 2026, 14:19

Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa wametakiwa kufuata taratibu za kisheria za umiliki wa ardhi pamoja na kusafisha na kuendeleza viwanja vyao ili kuepuka hasara za kiuchumi zinazoweza kujitokeza kutokana na kupoteza umiliki wa maeneo hayo.

Hayo yameelezwa na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa leo Juni 22, 2026, ofisini kwake alipokuwa akizungumza na Ruangwa FM Radio.Amesema kuwa mmiliki wa kiwanja anayeshindwa kukiendeleza au kukifanyia usafi ndani ya muda uliowekwa kisheria anaweza kupoteza haki ya umiliki, ambapo ardhi hiyo inaweza kurejea serikalini na hivyo kusababisha hasara ya kiuchumi kwa mhusika.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Ardhi Wilaya ya Ruangwa, Isihaka Panja, amewataka wananchi kuendeleza maeneo yao kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa, ikiwemo kuomba vibali maalumu vya ujenzi kupitia Ofisi ya Ardhi ya Wilaya kabla ya kuanza ujenzi.

Aidha, Panja amesema ujenzi unaofanyika bila kibali unaweza kusababisha athari za kiuchumi kwa mhusika, ikiwemo kulazimika kubomoa majengo yaliyojengwa kinyume cha sheria.

Ikumbukwe kuwa nchini Tanzania, suala la kufutwa kwa haki ya umiliki wa ardhi kutokana na kutokuendelezwa linaongozwa na Sheria ya Ardhi, Sura ya 113. Kifungu cha 45(3)(b) cha Sheria ya Ardhi kinaeleza kuwa haki ya kumiliki au kuhodhi ardhi (Right of Occupancy) inaweza kufutwa iwapo ardhi husika itaachwa bila kuendelezwa au kutumika kwa kipindi kisichopungua miaka miwili.