Nje ya mazao ya ufuta na korosho hakuna halimashauri za Ruangwa,Liwale,na Nachingwea
Ruangwa FM

Nje ya ufuta na korosho hakuna halmashauri za Ruangwa, Liwale na Nachingwea

20 April 2023, 10:31 pm

Mkuu wa wilaya ya Ruangwa katika mkutano mkuu wa sita RUNALI. Picha na Juma Mweru.

Na Loveness Daniel

Mkuu wa wilaya ya Ruangwa Mhe. Hassan Ngoma amewataka wakuu wa wilaya zote zinazounda ushirika wa chama kikuu cha RUNALI kusimamia kwa umakini na kuweka jitihada kubwa katika zao la korosho na ufuta katika halmashauri zao kwani mazao hayo ameyataja kuwa na asilimia 95 ya mapato ya ndani katika halmashauri zote zinazounda RUNALI.

DC Ngoma ameyazungumza hayo katika mkutano mkuu wa 6 wa chama kikuu cha Runali akiwa ndiye mgeni rasmi wa mkutano huo  ambao umefanyika April 20 2023 katika ghala la Runali wilayani hapa huku akiwasisitiza wakurugenzi wa halmashauri za Ruangwa, Nachingwea na Liwale kuwasimamia na kutetea maslahi ya wakulima  ili kudumisha uhai wa halmashauri zao.

‘’Nje ya mapato ya ufuta na korosho hakuna halmashauri ya Liwale ,Ruangwa wala Nachingwea mazao hayo ndio maisha kwenye halmashauri zetu hivyo ma DC tunapaswa kuwekeza nguvu kubwa katika kuwatizama na kuwasaidia wakulima kwani wakishindwa kuzalisha halmashauri zitayumba’’, amesema DC Ngoma.

‘’Nje ya mapato ya ufuta na korosho hakuna halmashauri ya Liwale ,Ruangwa wala Nachingwea mazao hayo ndiyo maisha kwenye halmashauri zetu hivyo wakuu wa wilaya tunapaswa kuwekeza nguvu kubwa katika kuwatizama na kuwasaidia wakulima kwani wakishindwa kuzalisha halmashauri zitayumba.’’

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Liwale Mhe. Goodluck Mlinga amewataka viongozi wa vyama vya msingi kuwa waaminifu katika malipo ya wakulima kwa kuwa atatumia vyombo vya dola pale itakapobainika viongozi hao “kupiga” fedha za wakulima.

Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mhe. Mohamed Moyo amewataka viongozi wa Amcos kuunda SACCOS zitakazosaidia kuweka akiba na kukopa ili  kuweza kusaidia kuwavutia wakulima wengi kujiunga katika vyama vya msingi kukwepa biashara ya kangomba inayowaumiza wakulima wengi, pia viongozi wa ushirika kujali maslahi ya mkulima ili kilimo cha mazao ya korosho, ufuta, alizeti na mbaazi kiwainue wakulima kwani ushirika ni biashara.

Sauti DC Liwale & Nachingwea

Kaimu mkurugenzi halmashauri wilaya ya Ruangwa DHRO Maisha Mtipa amesema ushirikiano wa vyama vya msingi na chama kikuu cha ushirika Runali ni jambo la msingi linaloimarisha na kustawisha halmashauri hizo hivyo amehimiza ushirikiano ili kuwahudumia wananchi kwa tija huku mkurugenzi wa wilaya ya Nachingwea Chihonda Kawawa amesema Runali inashiriki maendeleo katika jamii jambo ambalo linakuza uchumi wa taifa la Tanzania.

Sauti DED