Radio Fadhila

watoto wa kike wanufaika na mradi wa SDA.

16 October 2024, 7:34 PM

Shule tano za sekondari kutoka Halmashauri ya Mji Masasi zinazonufaika na mradi wa shirika lisilo la kiserikali la Sports Development Aid wametoa Shukrani kwa mradi huo ambao umekua chachu ya mabadiliko Chanya katika kuwajenga vijana katika maadili,uelewa na kujiamini hali iliyochangia kuongeza ufaulu kwa Watoto wakike katika shule mbalimbali zilizonufaikiwa na mradi huo.

Wameyasema hayo katika kikao kilichofanyika katika shule ya sekondari ya wasichana ya Masasi,kikiwa na lengo la kufanya tathimini ya kufika ukingoni mwa mradi na kuweza kutoa mawazo na mitazamo ambayo kwa kiasi kikubwa imeleta mabadiliko Chanya kwa wanafunzi wa kike katika shule za sekondari zikiwemo Chanikanguo,Mtandi Sululu,Mtapika na Anna Abdalah.

Hata huvyo wakati wa kikao hicho wadau hao waliliomba shirika hilo kupanua wigo katika shule zingine ili nazo ziweze kunufaika na mafunzo yanayotolewa na mradi huo kwani ni shule Hamsini (50) tu kutoka mkoa wa Mtwara zimenufaika na mradi huo.

Naye mshauri mwelekezi wa mradi huo Ndg. Hanif Tuwa amewataka wadau hao kuyaendeleza yale yote waliyojifunza kwa kuendeleza shughuli zilizotokana na mradi huo na kuzisambaza maeneo mbalimbali ambayo hayajafikiwa na mradi,huku akisisitiza kuwa mradi huo haujafutwa bali unafika mwisho ili kukaribisha miradi mingine.

Sambamba na hilo meneja wa mradi huo Bi.Jackline Mpunjo amesema mradi ulilenga kuwawezesha mabinti kupaza sauti zao kutokana na changamoto mbalimbali wanazozipitia ikiwemo ufaulu mdogo,mimba za utotoni Pamoja na utoro,kupitia mafunzo mbalimbali yaliyotolewa kwa makundi ya wanafunzi yameweza kuwapa kujiamini na kuweza kueleza changamoto mbalimbali wanazopitia.