Radio Fadhila
Radio Fadhila
19 May 2025, 11:28 AM

Mradi wa Kituo cha Biashara Masasi (Masasi Comercial Complex) umelenga kuboresha huduma kwa jamii na wafanyabiashara ndani na nje ya wilaya ya Masasi
Na Neema Nandonde
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kujenga Kituo cha Biashara Masasi (Masasi Commercial Complex) katika halmashauri ya Mji wa Masasi mkoani Mtwara.
Ametoa pongezi hizo Mei 18, 2025 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa mradi wa huo, ambapo amesema kuwa kituo hicho kitarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi sehemu moja, ikiwemo huduma za kifedha.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi huo Godfrey Mkumbo, amesema jengo hilo la biashara linakadiriwa kugharimu jumla ya Shilingi 2,711,652,080.22 hadi kukamilika kwake, ambapo tayari kiasi cha Shilingi 1,450,718,159.94 kimeshatumika na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.
Ukiwa katika Halmashauri ya Mji Masasi, Mwenge wa Uhuru umekagua miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tatu na kukimbizwa umbali wa km 78.0, ambapo umepitia miradi sita (Miradi miwili imezinduliwa, miradi miwili imewekewa mawe ya msingi na miradi miwili imekaguliwa).


Mwenge wa Uhuru umehamasisha wananchi juu ya mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI, Malaria, Rushwa, Madawa ya kulevya na Lishe, ambapo kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 ni, “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani n a Utulivu ”.