Radio Fadhila
Radio Fadhila
17 May 2025, 5:39 PM

Kampeni ya NBC Shambani inatarajia kuanza rasmi juni 1 na itahitimishwa Julai 31 2025, ambapo wanaojihusisha na biashara ya kilimo ambao ni wateja wa NBC, watakaokidhi vigezo watapatiwa zawadi
Na Neema Nandonde
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), imezindua rasmi kampeni ya NBC Shambani msimu wa tatu, inayolenga kuwezesha na kufanikisha shughuli za kilimo kwa wadau wote walioko kwenye mnyororo wa kilimo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Uzinduzi huo umefanyika Mei 16, 2025 ambapo umewakutanisha viongozi wa serikali, viongozi wa vyama vya msingi na ushirika, wafanyabiashara, maafisa ushirika na wakulima katika ukumbi wa Rock City Masasi huku kaulimbiu ya kampeni hiyo ikisema “wekeza shambani ushinde”.
Akihutubia kabla ya uzinduzi huo, mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Alphaxad Etanga, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rachel Kassanda, ameipongeza benki ya NBC kwa namna inavyofanya biashara kwa ukaribu na wakulima, huku akiitaka kuendelea kubuni njia mbalimbali za kuwainua wakulima.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU Alhaj Azam Mfaume, ameipongeza benki ya NBC kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa wakulima, huku akiwaomba kuendelea kuboresha mifumo kwenye maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake Meneja wa benki ya NBC Tawi la Masasi Andrew Hossa, amesema kuwa benki hiyo iko tayari kushirikiana na viongozi wa vyama vya msingi na ushirika wilayani humo, ili kutatua changamoto mbalimbali za wakulima zinazokwamisha kufikia malengo yao.
Kampeni ya NBC Shambani msimu wa tatu, inatarajia kuanza rasmi juni 1 na itahitimishwa Julai 31 2025, ambapo wanaojihusisha na biashara ya kilimo ikiwemo wasambazaji wa pembejeo za kilimo, wakulima, wasafirishaji,, wavuvi, wafugaji ambao wana akaunti za NBC, watakaokidhi vigezo watapatiwa zawadi ikiwemo pikipiki na kompyuta mpakato.