Radio Fadhila

UNESCO yaja  na  mradi  wa  kuwainua  vijana  Masasi

10 May 2025, 8:51 AM

Mratibu wa mradi Bridge Tanzania kitaifa Bi Fatma Shabani Mrope. Picha na Google

mradi huu utatekelezwa  kwa kipindi cha miaka mitano katika wilaya tatu ambazo  ni Masasi, Geita na Kaskazini Unguja, pia unawapa nafasi hawa Vijana na haswa Wanawake ni kwa asilimia 55% na Wanaume asilimia 45%

Na Neema Nandonde

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya UNESCO ya Nchini Korea – Korea National Commission for UNESCO (KNC- UNESCO), inatarajia kutekeleza Mradi wa Bridge Tanzania unaolenga  kuwainua  vijana  ambao wamekosa  kuingia  kwenye  mfumo rasmi  wa  elimu   na wanaishi katika mazingira magumu ili kuwainua  kiuchumi.

Akizungumza  na  redio Fadhila May 8, 2025 Mratibu wa mradi huo kitaifa Bi Fatma Shabani Mrope amesema, mradi huo utatekelezwa  kwa kipindi cha miaka mitano katika wilaya tatu ambazo  ni Masasi, Geita na Kaskazini Unguja, pia unawapa nafasi hawa Vijana na haswa Wanawake ni kwa asilimia 55% na Wanaume asilimia 45%.

Amefafanua kuwa mradi huo unatarajiwa kuwafikia  vijana  1,000 kutoka  kila  wilaya,  huku miongoni mwa vigezo ikiwa  ni  pamoja  na kijana  kuwa  na  umri  wa  kuanzia  miaka 16 hadi 30.

Amesisitiza  kuwa, kwa  kushirikiana  na  wilaya  lengwa, wataangalia  namna  ya  kupata  vigezo rahisi  vya  kuwapata  vijana  hao ili kusiwe  na  ugumu  wa vijana  kuitumia  apasavyo fursa  hiyo.

Ameongeza kuwa Shirika kwa Kushirikiana na Halmashauri itahakikisha Vijana wanatambulika na hatimaye kuwakutanisha na Wataalamu mbalimbali na kuwapatia maarifa stahiki kupitia Mradi huo yatakayowawezesha Vijana kuanzisha Miradi ya Kiuchumi.

Sauti ya 1 ya Mratibu wa mradi Bridge Tanzania kitaifa Bi Fatma Shabani Mrope.

Aidha Bi. Fatma amewataka  vijana  kujitokeza  kwenye mradi huo, kwakuwa watakaopata nafasi hiyo, muda  wa mafunzo hautaathiri shughuli zao nyingine wanazozifanya , huku akisisitiza kuwa wakati wa mafunzo watawezeshwa na  tume kupata chakula  cha mchana.

Sauti ya 2 ya Mratibu wa mradi Bridge Tanzania kitaifa Bi Fatma Shabani Mrope.

Mradi wa Bridge Tanzania umelenga moja kwa moja  kuwawezesha Vijana waliotengwa na wanaoishi katika mazingira  magumu katika jamii kupata Stadi za Maisha zitakazowawezesha Kuboresha hali zao za kiuchumi