Radio Fadhila

DC Kasanda awataka wazee kusimamia nidhamu na maadili kwa jamii

19 April 2025, 12:18 PM

Picha na Godbless Lucius

Wazee na viongozi wa dini nahitaji ushirikiano wenu juu ya kujenga maadili na nidhamu kwa wananchi, ili kujenga kizazi bora chenye heshima

Na Neema Nandonde

Mkuu wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Rachel Kassanda, amewataka wazee maarufu, viongozi wa dini na wazee wa mila wilayani humo  kusimamia maadili na nidhamu kwa wananchi katika maeneo yao, ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.

Akizungumza katika kikao na wazee maarufu, viongozi dini na wazee wa kimila kilichofanyika April 16, 2025 Mkuu wa Wilaya ya Masasi Kassanda amesema kuwa ushirikiano na wazee na viongozi wa dini katika kujenga maadili ni muhimu sana.

Aidha amewataka wazee na viongozi wa dini kuongea na kuwasisitiza waumini na wananchi wote makanisani, misikitini na mikutano ya kimila, kuhusu umuhimu wa lishe na kufanya kilimo cha mazao ya chakula kwa ajili ya afya, huku akiongeza kuwa zao la korosho sio kwa ajili ya biashara tu bali ni zao muhimu pia kwa lishe.

Vile vile amewataka kuhimiza amani na utulivu katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu, ili kutoharibu amani tuliyonayo kwa miaka mingi.

Wakizungumza katika kikao hicho, wazee hao wamesema watatoa ushirikiano wa dhati kwa viongozi, ili kuimarisha maadili kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.