Radio Fadhila
Radio Fadhila
11 April 2025, 2:41 PM

Wazazi wengi huwapeleka watoto kwa ndugu akiwemo bibi au babu, pasi na kufuatilia maendeleo ya watoto hao au kuwapatia mahitaji muhimu, jambo linalosababisha watoto kutoangaliwa ipasavyo na ndugu walioachiwa, na hatimaye kujikuta wanajitafutia chakula, makazi na malazi mtaani.
Na Neema Nandonde
Imeelezwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la watoto wa mitaani wilayani Masasi mkoani Mtwara, ni baadhi ya wazazi kuwatelekeza watoto kwa bibi zao au kwa ndugu wengine, badala ya kuwalea wao wenyewe.
Hayo yameelezwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Masasi Leila Kasugulu alipokuwa akizungumza na Redio Fadhila kupitia kipindi cha Fadhila Mseto, April 11, 2025 kuhusu maadhimisho ya wiki ya mtoto wa mtaani.
Amesema wazazi wengi, huwapeleka watoto kwa ndugu akiwemo bibi au babu pasi na kufuatilia maendeleo ya watoto hao au kuwapatia mahitaji muhimu, jambo linalosababisha watoto hao kutoangaliwa ipasavyo na ndugu walioachiwa na hatimaye kujikuta wanajitafutia chakula, makazi na malazi mtaani.
Amesema sababu nyingine ni ulevi uliopindukia wa wazazi au walezi, wazazi au walezi kufariki, wazazi kutengana na kwa asilimia chache ni tabia ya utukutu wanayokuwa nayo watoto wenyewe hali inayosababisha watamani kuishi maisha huru mitaani.
Sauti ya Afisa maendeleo ya Jamii halmashauri ya mji Masasi Leila Kasugulu
Aidha ameeleza kuwa halmashauri ya mji Masasi, inaendelea na jitihada za kuwaondoa watoto hao mitaani kwa kuwapeleka kwa walezi wa kuaminika, wanaochaguliwa na idara ya ustawi wa jamii na mashirika au taasisi nyingine binafsi zinazotetea haki za watoto, au kuwapeleka kwenye vyuo vya ufundi ili waweze kujipatia ujuzi utakaowasaidia kujipatia kipato halali.
Kilele cha maadhimisho hayo kitaifa, kitafanyika April 12, 2025 katika viwanja vya VETA mkoani Mtwara ambapo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wananawake na Makundi Maalum Dkt. Doroth Gwajima, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo.