Radio Fadhila
Radio Fadhila
19 March 2025, 10:55 AM

Mkurugenzi wa Huduma kwa wateja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Masasi Nachingwea (MANAWASA) Obadia Mtuya. Picha na Godbless Lucius
“Wateja wa huduma ya maji wanazidi kuongezeka, na sisi kama taasisi tutaendelea kuboresha mifumo yetu ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora, na kuziba kabisa mianya ya ubadhirifu na kumfanya mteja awe salama anapotumia huduma za maji”
Na Neema Nandonde
Katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira, kuondoa malalamiko ya wateja kuhusu kubambikiziwa ankara za maji na changamoto ya wateja kulimbikiza ankara za maji, Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Masasi Nachingwea (MANAWASA), imefanikiwa kufunga mita za maji 95 za malipo ya kabla kwa baadhi ya wateja zikiwemo taasisi.
Akizungumza Machi 18, 2025 kupitia kipindi cha Morning Booster kinachorushwa na redio Fadhila, kuelekea kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji, Mkurugenzi wa Huduma kwa wateja MANAWASA Obadia Mtuya amesema kuwa, wameanza kufunga mita hizo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambalo pia litasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha ameongeza kuwa maeneo mengine yaliyoboreshwa ni pamoja na kituo cha kisasa cha miito ya simu kwa wateja cha bure na mifumo ya usomaji na ulipaji wa ankara za maji.
Sambamba na hayo, Mtuya amewasihi wananchi wilayani Masasi kushirikiana na MANAWASA katika kulinda vyanzo vya maji na kufichua wahujumu wa miundombinu ya maji huku akiwasisitiza kulipa ankara za maji kwa wakati, ili mamlaka hiyo iweze kujiendesha na kupanua mtandao wa maji kwa wateja wengine.