Radio Fadhila
Radio Fadhila
13 March 2025, 6:33 AM

Tukio hilo lilitokea Februari 12, 2025, mtuhumiwa alimpiga mama yake kichwani kwa kutumia mchi, na kusababisha majeraha yaliyosababisha kifo chake.
Na Neema Nandonde
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia Hamisi Mohamedi (25), mkazi wa Kata ya Mlingula, Wilaya ya Masasi, kwa tuhuma za mauaji ya mama yake mzazi, Aidina Rashid (56).
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Machi 12, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, SACP Issa Suleimani, amesema tukio hilo lilitokea Februari 12 mwaka huu, ambapo mtuhumiwa alimpiga mama yake kichwani kwa kutumia mchi, na kusababisha majeraha yaliyosababisha kifo chake.
Chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na imani za kishirikina.
Aidha, Jeshi la Polisi linamshikilia Salumu Liyove, mkazi wa Kata ya Libobe, kwa tuhuma za kuzini na mtoto wa mdogo wake, ambapo inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimchukua mtoto huyo kwa lengo la kumsomesha, baada ya kuona wazazi wake wakikabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Sambamba na matukio hayo, Kamanda Suleimani amesema kuwa Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa 29 kwa makosa mbalimbali, wakiwemo watuhumiwa 10 waliokamatwa na pombe haramu ya gongo lita 90.
Wengine ni watuhumiwa 15 waliokamatwa na kilo 366 za bangi, misokoto 57, na kete 86 za dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa bangi na Pia kuna watuhumiwa wanne waliokamatwa kwa makosa ya wizi.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limewataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia vyombo vya sheria kuwasilisha malalamiko yao.