Askofu wa jimbo la Tunduma awataka watu kumrudia Mungu
9 December 2024, 11:20 AM
Waamini wamekumbushwa kuwa sauti ya matumaini kama Nabii Baruku alivyokuwa sauti ya matumaini na kualikwa ili waweze kubadilika.
Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la TUNDURU-Masasi, Mhashamu Askofu Filbert Felician Mhasi kwenye homilia ya Ibada ya Misa Takatifu ya Dominika ya 2 ya Majilio ambayo wanovisi 13 wamefunga nadhiri zao za kwanza iliyofanyika kwenye Nyumba ya Malezi ya Mtakatifu Yosef – Namiungo, jimboni TUNDURU-Masasi.
Askofu Mhasi amewambia waamini kuwa Nabii Baruku aliwakumbusha wale Waisraeli kuwa waanze kufurahi kwani waliondoka kwa miguu tena kwa aibu kwenda utumwani na kuwaambia wafurahi kwani watarudi kwa furaha.
Aidha ameeleza kwamba walipelekwa utumwani kwa sababu Waisraeli hawakutii na kwa sasa hayo ndiyo yanayotumika siku hizi katika ulimwengu huu na kuwasihi waamini kufuata sheria na miongozo iliyoweka iwe na jamii, kanisa au shirika.
Hata hivyo amewataka waliomba na kufunga Nadhiri za kitawa kama walivyoomba kwa unyenyekevu, wanapaswa waishi hivyo na kufuata miongozo na kumruhusu Bwana kuishi mioyoni mwao.
Amebainisha kwamba wale ambao muda wote watamrudia Bwana na kukaa naye daima hawatahangaishwa na vitisho au jambo lolote.
Askofu Mhasi amewataka kuwa watii na waadilifu na kushika sheria na miongozo kwani kufanya hivyo watakaa na Bwana, kwani Mwenyezi Mungu anawapenda na anakaa na watu wake.
Amewatahadharisha kuwa makini na ulimwengu huu na kuanza na Bwana kwani kuishi hivyo hawatakuwa na shida hasa katika maangaiko ya kiuchumi yaliyopo siku hizi.
“Mbaki katika taratibu na miongozo na mengine yote yatakuja tu! na daima watiini wakubwa wenu la sivyo mtakula chuma na achaneni na mambo ya starehe”, amesema Askofu Mhasi.
Amewaomba wachague kilicho chema ili wasiwe kichekesho kwa Mungu na kwa watu na kuwa sauti ya matumaini kwa wengine.
Amewaomba na kuwataka wasikate tamaa.