Wapigwa msasa utambuzi, utunzaji wa alama muhimu kwenye noti za Tanzania
11 September 2024, 5:44 PM
Utambuzi wa noti halali
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mtwara imetoa elimu ya namna bora ya utunzaji wa noti pamoja na utambuzi wa alama muhimu za usalama katika noti za Tanzania kwa watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Lengo ni kuhakikisha kwamba watanzania wote wanazifahamu alama hizo za usalama ili kuepukana na fedha bandia ambazo zimeanza kupanda kasi katika mzunguko wa kifedha.
Amesema “Ni muhimu kwa wananchi kuzitambua alama halisi zinazopatikana kwenye noti halali za Tanzania ili kuepuka utapeli wa kupewa noti bandia na hasa katika kipindi hiki cha ununuaji na uuzaji wa mazao na pia mifugo kutoka kwa wakulima na wafugaji.”
Ameongeza kuwa ni vyema sasa wafanyabiashara wakawa na vifaa maalum vinavyoweza kutambua noti halali na bandia ambapo ni pamoja na taa maalum zenye mwanga wa zambarau (Utraviolet light bulb) kwa kuwa taa hizo zina uwezo wa kutambua alama muhimu zilizo katika noti halali ambazo si rahisi kuzitambua kwa macho ya binadamu pasipo vifaa hivyo.
Kwa upande wa utunzaji wa noti za Tanzania watumishi hao wameshauriwa kuzingatia utunzaji bora wa noti hizo kwa kuepuka kuzishika katika hali ya unyevunyevu, kuzikunjakunja au kufinyanga mkononi, wasihifadhi kwa kuchimbia ardhini, kuweka noti kwenye nguo za ndani au kuzifunga kwenye kanga, wasiweke noti kwenye soksi, viatu na chini ya godoro.