Radio Fadhila

DC Masasi aongoza kikao cha dharura kujadili ugonjwa wa mlipuko

22 June 2024, 5:47 PM

Mkuu wa Wilaya ya Masasi Lautel John Kanoni ameongoza kikao cha dharura kilichowakutanisha vyombo vya ulinzi na usalama wilaya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Afya Halmashauri ya Wilaya Masasi na kujadiliana kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa kuharisha na kutapika katika kijiji cha Mbagala kitongoji cha Miesi kata ya Lupaso.

Akitoa taarifa ya hali ilivyo Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) Ruben Mwakilima amesema “katika uchunguzi wetu kulikua na kaya 74 na kati ya hizo kaya 24 pekee zilikua na choo, na tukumbuke eneo lile lina watu wengi na zaidi ya asilimia Hamsini ni wahamiaji kutoka Wilaya za Jirani ambao wamekuja kulima zao la Ufuta”.

“Hali hiyo imepelekea kuwepo na idadi kubwa ya watu ambapo kwa makadirio tuliyoyapata siku hiyo ni watu 993 na eneo walilopo ni ambalo linakosa maji na maji wanachota kwenye mito kuanzia mto miesi na hayo ndio ya kunywa na bahati mbaya wengi wao hawachemshi ambapo wangeweza kuua vimelea.”

Katika hatua nyingine kuhusu Matibabu Amesema “Wagonjwa Mwanzo walikua wanakwenda zahanati ya Utimbe na ndiko tulipobaini lakini kwa sasa tumeanzisha Kambi ambayo inayo wataalamu watatu kwa sasa na kile tulichokifanya kimeleta matunda na kupunguza idadi ya wagonjwa”.

Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa wananchi wasio na vyoo waweze kuchimba na ifikapo Julai 20,2024 kila kaya iwe na choo na hatua nyingine muhimu za afya ziweze kufuatwa.