Lishe kwa watoto wenye umri wa miaka 3-5
17 February 2021, 10:09 AM
Watoto katika umri huu wana mahitaji makubwa ya virutubishi kwa sababu wapo katika kipindi cha ukuaji wa haraka.
Pia katika kipindi hiki huwa hakuna uangalizi mzuri wa watoto, na hivyo kuwaacha watoto wale chakula peke yao au kula na watoto wakubwa hivyo kushindwa kupata virutubishi vya kutosha ili kukidhi mahitaji ya miili yao. Katika umri huu mtoto anaweza kuachishwa kunyonya na kuendelea kula chakula cha familia katika uwiano wa makundi matano ya vyakula ili kupata virutubishi vya kutosheleza mahitaji yake ya mwili kilishe.
Vyanzo vingine vyenye virutubishi vingi kwa mfano vyakula vya asili ya wanyama kama vile maziwa ya ng’ombe lazima yajumuishwe katika mlo wa mtoto hadi miaka mitano.Walezi wa watoto wenye umri wa miaka 3–5 wanatakiwa:Kuendelea kupewa maziwa, kwa mfano ya ngo’mbe, kama sehemu ya chakula cha mtoto. Kuwapa chakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote matano ya vyakula.
Kuwapa milo mitatu kwa siku.Kuwapa asusa angalau mara mbili kwa siku (katikati ya mlo na mlo) kwa mfano uji, maziwa, kipande cha mhogo uliochemshwa au viazi vitamu kulingana na mazingira na kinaweza kuwa chakula kilichobaki kutoka katika mlo wa familia.Wasilazimishe mtoto kula.
Tumia mbinu shirikishi za ulishaji ili mtoto aweze kukubali kula. Kuhakikisha mtoto anapewa maji na chakula safi na salama. Kuhakikisha vyakula anavyopewa mtoto vinatayarishwa na kuhifadhiwa vizuri ili kuzuia maambukizi yanayoweza kusababisha magonjwa kama vile kuharisha.
Kuwapeleka watoto kliniki kwa ajili ya ufuatiliaji wa maendeleo, kupewa chanjo zote kama miongozo ya kitaifa inavyoelekeza. Kutumia chumvi yenye madini joto wanapoandaa chakula cha mtoto. LISHE KWA WATOTO WENYE UMRI WA MIAKA 6–10 Watoto katika umri huu wana mahitaji makubwa ya virutubishi kwa sababu bado wanaendelea kukua na bado wanawategemea watu wengine kuwalisha. Pia kipindi hiki watoto hawa hufanya shughuli nyingi zinazohusisha mwili kama kucheza michezo mbalimbali pamoja na ukuaji wao ambavyo kwa pamoja huongeza mahitaji ya virutubishi ili kukidhi mahitaji ya miili yao.
Vilevile katika kipindi hiki watoto wengi huwa wameanza shule na hivyo wanaweza kukosa mlo wa mchana lakini pia wanakabiliwa na hatari ya kupata magonjwa yanayotokana na kutumia maji yasiyo safi na salama. Hali hizi zote huchangia uwezekano wa kupata utapiamlo.