Care International yawafikia wasichana 600 Mufindi DC
11 October 2024, 22:00
Na Mwanaid Ngatala.
Ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani leo Oktoba 11, 2024, shirika lisilo la kiserikali, Care International, kupitia mradi wa Pesa yake maisha yake (Her Money Her Life), limegawa taulo za kike na sabuni kwa wasichana wapatao 600, katika shule ya msingi Kasanga na Igowole sekondari wilayani Mufindi.
Hayo yamefanyika katika hafla ya maadhimisho ya mtoto wa kike duniani katika halmashauri ya wilaya ya Mufindi, yenye kauli mbiu isemayo “Mtoto wa kike na uongozi, tumshirikishe wakati ni sasa”.
Sherehe hizo zimeambatana na shuguli mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu ya lishe,ukatili wa kijinsia,na uongozi bora, kwa kushirikiana na uongozi wa halmashauri ya wilaya na Mufindi na shirika la World Vision Tanzania.
Mtoto wa kike ana haki ya kushiriki shughuli mbalimbali wazazi na walezi ni jukumu la kila mmoja, kuwalinda ili watimize ndoto zao za baadae.
Katika kuingazia siku hii ya mtoto wa kike duniani, kupitia kipindi Cha Morning Gia kinachoruka kupitia Mufindi FM 107.3, imeeleza kwamba, Jitihada za kumsaidia mtoto wa kike kuondokana na changamoto zinazomkwamisha kushiriki katika katika nafasi za uongozi zinapaswa, kuanzia ngazi za familia.
Afisa Mradi wa Children’s Villages (SOS), Wilaya ya Mufindi, Bw. Benson Rwakatale, ameiasa jamii kuyatazama na kuyabadili mambo ambayo yanamkandamiza mwanamke katika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya kielimu na Kisiasa.
Aidha kufuatia jitihada hizo mbalimbali za kumuinua Mtoto wa kike, Bw. Bensoni amewaomba wanawake wasibweteke na kwamba ndio wakati wao wa kuweza kupata haki za msingi kama ilivyo kwa mtoto wa kiume.
Maadhimisho haya yanajiri ikielezwa kuwa matatizo ndani ya familia yanachangia kwa kiasi kikubwa matunzo mabaya kwa watoto ambapo asilimia 22 ya wasichana wenye umri wa miaka 15-19 walipata ujauzito kwa mwaka 2022 huku mikoa vinara wa ndoa za utotoni ikiwa ni Songwe, Ruvuma, Katavi, Rukwa na Mara.
MWISHO