Wahamiaji haramu 16 mbaroni wakisafirishwa kwa STL
9 April 2024, 10:09
Na Jackson Machowa-Mufindi
Jeshi la polisi kwa kushirikiana na idara ya uhamiaji mkoani Iringa linawashikilia wahamiaji haramu 16 raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali kinyume cha sheria.
Wahamiaji hao wamekamatwa Jumamosi ya tarehe 6 April 2024 katika eneo la msitu wa Luganga kata ya Ifwagi hapa wilayani Mufindi baada ya dereva wa gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Land Cruiser V8 lenye namnba za usajili T803 CVW kulitelekeza gari hilo baada ya kugundua anafuatiliwa na jeshi la polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari, kamanda wa jeshi la polisi mkoani Iringa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa jeshi hilo SACP Allan Bukumbi amesema awali gari hilo lilikuwa likitambulika kwa namba za usajili bandia STL 3999 huku dereva na mmiliki wa gari hilo wakiendelea kumtafutwa.
Aidha kamanda Bukumbi amesema jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wengine 13 kwa makosa ya wizi na kusafirisha vipodozi vilivyopigwa marufuku vyenye viambata vya sumu huku akisema kuwa watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji ACI Peter Kimario amewataka wananchi kuwa makini na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona watu wasiowafahamu.