Tani 124.1 za mbaazi zauzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani
11 October 2023, 12:34
Mfumo wa stakabadhi ghalani umewezesha kuuza mbaazi shilingi 1,710 kwa kilo huku wakulima wakifurahia mfumo huo na kuridhia bei.
Na Jackson Machoa/ Morogoro
Jumla ya tani 124.1 za zao la mbaazi zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 212 zimeuzwa katika mnada uliendeshwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani katika ghala kuu la kuhifadhi mazao ya nafaka lililopo kijiji cha Misegese wilayani Malinyi mkoani Morogoro.
Mnada huo uliofanyika mubashara kwa njia ya mtandao huku ukishuhudiwa na mamia ya wakulima waliofika kuuza mbaazi zao ulionyesha bei ya juu ya soko kuwa ni shilingi 1710 kwa kilo, bei ambayo iliridhiwa na wakulima na hivyo kuruhusu mnada kufanyika.
Akizungumza na wakulima wa zao hilo mnadani hapo, afisa ushirika wilayani humo Bwana Malick Mabuba amesema mfumo wa stakabadhi ghalani unalenga kumwepusha mkulima dhidi ya unyonywaji unaofanywa na wafanyabiashara wasio waadilifu kwani mfumo huo humwezesha mkulima kuuza mazao yake kwa bei ya soko.
Katika hatua nyingine Bwana Mabuba amesema halmashauri kwa kushirikiana na vyama vya ushirika wanaandaa utaratibu wa kuagiza mbegu fupi za mbaazi zitakazo komaa kwa haraka ili kuendana na msimu wa zao hilo sawa na maeneo mengine.
Huu ni mwendelezo wa mfumo wa stakabadhi ghalani kuendelea kutumika katika uuzaji wa mazao mbalimbali ya wakulima kwa njia ya minada wilayani humo ambapo wakulima hukubaliana na kuuza mazao yao kwa pamoja.