Aboud Ziarani Iringa
11 October 2023, 11:19
Na KEFA SIKA/MUFINDI.
Mlezi wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa Ndugu Mohamed Aboud Mohamed amewataka wananchi Wilayani Mufindi kufanya kazi kwa bidii kwani Serikali inaendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Mhe. Aboud ameyasema hayo katika ziara ya kutembelea mashina ya Chama hicho, kwenye Wilaya ya Mufindi na kuahidi kuwa changamoto zote zitatuliwa ikiwemo changamoto ya ukosefu wa maji safi.
Awali akimkaribisha Mlezi huyo Wilayani Mufindi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi Bw. George Kavenuke amesema kuwa miradi ya Serikali inaendelea kutekelezwa ikiwemo mradi wa maji katika kata ya Mbalamaziwa ambao utasaidia vijiji 20.
Baada ya ziara hiyo Katibu Mwenezi wa Chama cha Mampinduzi wilaya ya Mufindi Bw. Dickson Lutevele amesema kuwa wamepokea maelekezo na wataenda kufanya maandalizi ya kutosha kuelekea kwenye uchaguzi mdogo wa mwaka 2024.
Wakisoma risala baadhi ya viongozi wa Chama hicho kwenye ngazi ya shina wamesema kuwa changamoto kubwa kwenye maeneo yao ni ukosefu wa ofisi za Chama, Ukosefu wa Elimu ya mfumo mpya wa kielektroniki wa kujisajili na uchelewaji wa kadi za wanachama.
Mlezi wa CCM Mkoani Iringa mhe. Aboud na Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya amefanya ziara leo katika Wilaya ya Mufindi na kufanya Mkutano na wananchama katika kata ya Boma, Kata ya Mbalamaziwa, kata ya Ikongosi sambamba na kata ya upendo.
Tar 11/10/2023 anafanya ziara kwenye wilaya ya kilolo na tarehe 12/10/2023 atahitimisha ziara yake katika manispaa ya Iringa.MWISHO.