Wananchi Mufindi wapewa elimu umiliki ardhi
11 September 2023, 12:46
Afisa mipango miji mkuu kutoka Wizara ya Ardhi Fabian Mtaka akizungumza na wananchi wa kijiji cha Idetero kata ya Mbalamaziwa wilayani Mufindi.Na Bestina Nyangaro
Kuwa na hatimiliki za ardhi kutasaidia kupunguza migogoro ya ardhi
Na Bestina Nyangaro-Mufindi
Idara ya Ardhi halmashauri ya wilaya ya Mufindi imetoa elimu kwa wananchi wilayani humo kuelekea kuanza kutekelezwa kwa mradi wa Uboreshaji Usalama wa Miliki za Ardhi.
Zoezi hilo limefanyika katika vijiji vya Idetero, Nyanyembe na Kitelewasi kata ya Mbalamaziwa, likiongozwa na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Fabian Mtaki ambaye ni afisa mipango miji mkuu kutoka Wizara ya Ardhi amesema lengo la mradi ni kumsaidia kila mtanzamia anayemiliki ardhi kuwa na hatimiliki ili kuona tija ya ardhi yake.
Steven Songoi na John Batega ni wawakilishi kutoka asasi za kiraia wameeleza kwa kila mwananchi apaswa kuwa na kitambulisho au namba ya kitambulisho cha uraia au barua ya utambulisho kutoka ofisi ya mtendaji.
Naye mpima ardhi mkoani Iringa Bw. Makuka Mkasa amewaasa wananchi kutatua migogoro miongoni mwao ili kurahisisha zoezi ndani ya muda uliyopangwa.
Afisa ardhi halmashauri ya wilaya ya Mufindi Bw. Simon Mbago, ameongeza kwamba, “Nawashauri wale ambao mna maeneo ya familia ya urithi gawaneni siku hizi tunasema kila mtu awe na chake ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kutokea huko mbeleni katika vizazi vyetu”.
Nao wananchi wamesema wapo tayari kuupokea mradi na kushauri kuchukuliwa kwa uzito fursa hiyo sanjari na kuacha maeneo ya njia zitakazoruhusu shughuli za kilimo na ufugaji kuendelea.
Mpango huo unatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii na kutekelezwa ndani ya muda wa miaka mitano ikiwa wilayani Mufindi zaidi vijiji 41 vitanufaika kwa ufadhili wa serikali bila mwananchi kuchangia kiasi chochote cha fedha.