Ileje FM

Diwani CCM afariki kwa kunywa maji ya betri

November 27, 2025, 6:22 pm

Aliyekuwa diwani kata ya Shiwinga wilayani Mbozi Lusekelo Mwalukomo enzi za uhai wake

kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Mbozi Hamad Mbega inadaiwa diwani huyo alifanya maamuzi ya kunywa maji ya betri kutokana na msongo wa mawazo.

Na Denis Sinkonde,Mbozi

Aliyekuwa diwani  mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Shiwinga, Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe Lusekelo Mwalukomo, amefariki dunia baada ya kunywa maji ya betri, tukio lililotokea Novemba 26, 2025 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mbozi Mission.

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Hamad Mbega akizungumza na mwananchi digital leo Novem,ba 27, 2025 kwa njia ya simu amethibitisha kutokea kwa kifo hicho huku akisema sababu zilizopelekea diwani huyo kunywa maji hayo bado hazijafahamika.

Mbega amesema taarifa za awali zinadaiwa ni msongo wa Mawazo lakini wataalamu wanaendelea kufuatilia kwa undani zaidi taarifa kamili zitatolewa juu ya nini kilichopelekea kunywa maji ya betri.

“Wataalamu wetu wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi maana alikutwa amekunywa maji ya betri Novemba 26, 2025 saa nne asubuhi madaktari walifanya jitihada za kuokoa uhai wake lakini hawakufanikiwa,” amesema Mbega. 

Mkuu huyo wa wilaya amesema anajiandaa Kwenda nyumbani kwa marehemu kukaa na familia ya marehemu pamoja na Chama cha mapinduzi ambako ni kiongozi pia diwani aliyetokana na chama hicho na tarifa ya taratibu za mazishi zitatolewa  baada ya kikao.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Mbozi Hamad Mbega

Hata hivyo baada ya kikao hicho mkuu huyo wa wilaya amesema.mazishi yanatarajia kufanyika Novemba 28, 2025 nyumbani kwake Shiwinga.

Akizungumza kutoka kijijini Shiwinga, baba wa marehemu Mchungaji Ambukege  Mwasomola, amesema mwanawe alianza kuugua wakati wa michakato ya uchaguzi  Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na mara kadhaa alilalamikia kuishiwa nguvu na kukosa hamu ya kula.

Amesema marehemu mwenyewe alimueleza mkewe kuwa amekunywa maji ya betri alipokuwa ametoka kununua mbolea, na alipelekwa hospitalini haraka mara baada ya hali yake kubadilika.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo, alisema hakuna taarifa yoyote ya tukio hilo iliyoripotiwa polisi.

“Sijaipokea taarifa hiyo, kama kweli angekunywa maji ya betri, kwa taratibu zilivyo lazima ingeripotiwa polisi ili kutolewa fomu kwa ajili ya matibabu ntaendelea kufuatilia, tukipata taarifa kamili tutaeleza,” alisema Kamanda Senga.