Ileje FM

Ileje wajipanga kukabiliana na udumavu

November 19, 2025, 12:26 pm

Mkuu wa wilaya ya Ileje Farida Mgomi akizungumza wakati wa kikao cha tathimi ya lishe robo ya tatu. (Picha na ofisa habari Ileje)

Na Denis Sinkonde, Ileje

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, ametoa wito kwa kina baba kushiriki kikamilifu katika masuala ya lishe ili kuhakikisha familia zinakuwa na afya bora na kupunguza udumavu kwa watoto.

Mgomi ametoa wito huo umetolewa Novemba 17, 2025  katika kikao cha tathmini ya Mkataba wa Lishe robo ya kwanza kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya uliopo Itumba.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mgomi alisisitiza kuwa jukumu la malezi na lishe bora si jambo la mama pekee, bali linapaswa kuwa wajibu wa wazazi wote wawili kwa pamoja.

Alisema kuwa ushiriki hafifu wa wanaume katika masuala ya lishe umekuwa ukisababisha changamoto mbalimbali zinazoweza kuzuilika endapo kutakuwepo nguvu ya pamoja kwenye familia.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Ileje Farida Mgomi

Mgomi amesema Umuhimu wa unyonyeshaji wa watoto wachanga na kina mama kuwapatia maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo pasipo kuchanganya na chakula kingine chochote

“Unyonyeshaji wa mara kwa mara unasaidia kuongeza kinga mwilini kwa mtoto, kuimarisha ukuaji wa ubongo na kupunguza hatari ya utapiamlo na kuwataka viongozi wa ngazi zote kuendelea kutoa elimu hiyo kwa jamii ili kuhakikisha watoto wa Ileje wanakua katika msingi bora wa kiafya,” amesema Mgomi.

Aidha, alizitaka kamati na wadau wa lishe katika ngazi za Kata na vijiji kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa jamii hasa kipindi hiki ambacho serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kupunguza kiwango cha udumavu nchini.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Ileje Farida Mgomi

Amesisitiza kuwa ni muhimu kila kaya kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili, ikiwemo vyakula vyenye virutubisho vya kujenga mwili, kulinda mwili na kutoa nguvu.