Ileje FM

Wakulima wapewa mbinu bora za uzalishaji kahawa Songwe

October 15, 2025, 9:44 am

Mkulima akiwa kwenye kichanja cha kuanikia zao la kahawa (Picha na Anord Kimbulu)

Na Anord Kimbulu, Songwe

Katika kuhakikisha kuwa zao la kahawa aina ya Arabika kutoka Nyanda za juu Kusini linaendelea kufanya vizuri kwenye soko la kimataifa, wakulima wa kahawa wilayani Mbozi mkoani Songwe, wameanza kunufaika na mafunzo ya kitaalamu pamoja na miche ya miti ya matunda na kivuli, hatua hii inalenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha ustahimilivu wa zao hilo.

Mafunzo hayo yametolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Solidaridad kwa kushirikiana na serikali , ambapo wakulima wamefundishwa mbinu za kilimo mseto za kuchanganya zao la kahawa na mazao mengine rafiki kwa mazingira, ambapo wakulima wakulima wamesema mbinu hizo zitaleta mabadiliko chanya kwenye mashamba yao.

Msimamizi wa mradi huo kutoka Solidaridad Roselaida Ngowi amesema miradi huo unalenga kuweza kuboresha uzalishaji, wa zao la kahawa ambapo  jitihada hizo zitasaidia kuboresha uzalishaji au kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao hilo kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo au mbinu bora za kilimo cha kahawa kwa wakulima.

Ngowi amesema katika kuboresha uzalishaji wa zao la kahawa wanawasaidia wakulima kuwafundisha teknolojia ambazo huwasaidia wakulima kuwa na ustahimilivu katika uzalishaji wa zao hilo na kutekeleza jitihada ambazo zinachangia kubadilisha mabadiliko ya tabia nchi.

Sauti ya msimamizi wa mradi Roselaida Ngowi

“Baada ya wakulima kupata mafunzo haya yatawasaidia kuelimisha jamii kwa ujumla kwani mradi huu pia unasaidia kuzalisha miti ya kivuli mafunzo haya yamewasaidia wakulima kupata elimu ya sahihi ya kupangilia miti ya kivuli katika mashamba ya kahawa na kupata tija,” amesema Ngowi.

Amesema mafunzo hayo yatawasaidia wakulima kurutubisha udongo, kurekebisha hali ya hewa ili kuleta ustahimilivu wa mazingira na kiuchumi katika sekta ya zao la kahawa kwa wakulima ndani ya mikoa ya Songwe na Mbeya na taifa kwa ujumla. 

Meneja wa Kituo cha Utafiti wa Kahawa (TACRI) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dismas Pangalas amesema mafunzo hayo yamejikita kubainisha, kupendekeza na kutoa muongozo wa aina ya miti inayofaa kuchanganya kwenye mashamba ya kahawa kwa lengo la kuweza kuleta kivuli kitakachowezesha kukabilia na hali  ya jua kali na ukame, hivyo wakulima wamepata fursa kujua,mpangilio sahihi unaofaa katika kupanda kahawa, sambamba na miti ya kivuli.

Amesema mafunzo hayo yameweka mkazo katika matumizi ya migomba kama chanzo cha kupata chakula na kipato.

Sauti ya meneja wa Tcri Dismas Pangalas
Kahawa aina ya Arabika inayozalishwa nyanda za juu kusini (Picha na Anord Kimbulu)

Kwa upande wake mkuu wa Divisheni ya Mifugo, Uvuvi na kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, George Nipwapwacha, amewapongeza wakulima kwa ushiriki wao na kuwasihi kutumia vyema elimu waliyopewa ili kuboresha maisha yao na kuongeza ushindani wa uzalishaji wa zao la kahawa ya Tanzania duniani.

Amesema wanawashukuru watu wa mradi Solidaridadi kwa kutoa mafunzo haya kwaniaba ya serikali na kwamba watayafanyia kazi kwa kushirikiana kati ya sekta binafsi na serikali na naamini mafunzo waliyopata wakulima watatekeleza kama walivyofundisha na kupata tija ya uzalishaji wa zao hilo.

Sauti ya mkuu division ya mifunzo na uvuvi George Nipwapwacha

 Akizungumza kwaniaba ya wakulima wengine Maria Mwazembe amesema kupitia kilimo mseto tumejifunza ukichanganya kilimo cha kahawa na miti ya kivuli pamoja na miti matunda  kama maparachichi na ndizi kunaweza kukupunguzia gharama ya kusimamia shamba .

Sauti ya mkulima Maria Mwazembe