Ileje FM
Ileje FM
September 18, 2025, 6:20 am

Na Denis Sinkonde,Songwe
Jeshi la Polisi mkoani Songwe linamtafuta Evacery Mwaweza mkazi wa Kitongoji cha Ululu kiijiji cha Idiwili kata ya Idiwili wilayani Mbozi mkoani Songwe kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Zabroni Mwambogolo (28) mkazi wa kitongoji hicho wakati wakiangalia mpira wa Simba na Yanga.
Akizungumzia tukio hilo jumatano ya Septemba 17,2025,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga amesema limetokea Septemba 16,2025 saa 12:50 jioni baada ya mabishano ya mpira wa Yanga na Simba.
Kamanda Senga amesema marehemu alijeruhiwa kwa kuchomwa kisu eneo la kifuani ambapo alifariki dunia wakati anapelekwa katika zahanati ya Iyula iliyopo wilayani humo kwa ajili ya matibabu.
Sauti ya kamanda wa polisi mkoa wa Songwe
“Jeshi la polisi mkoa wa Songwe linatoa wito Kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kutojohusisha vitendo vya vurugu vinavyoweza kusababisha madhara makunwa ikiwa ni pamoja na upotevu wa maisha hususani mabishano yakiwepo ya michezo,” amesisitiza kamanda Senga.
Katika tukio linguine kamanda Senga amesema watu watatu wamefariki Dunia katika ajali iliyohusisha bajaji na gari katika barabara kuu ya Tunduma_Sumbawanga eneo katika kata ya Chipaka Tarafa ya Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe.
Kamanda Senga amesema gari lenye namba za usajili T.525 ACB aina ya Canter ikiwa inaendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina lake aligonga bajaji yenye namba za usajili MC 308 EXE iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina Silasi Malongo(23) mkazi wa Mwaka Tunduma.