Radio Fadhila
Radio Fadhila
11 April 2025, 2:52 PM

Mhandisi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Mashariki Khatibu Chande, alipokuwa akizungumza kupitia redio Fadhila. Picha na Godbless Lucius
Namba 15040 mwananchi ataitumia kuripoti namba za mtu anayejihusisha na utapeli wa kimtandao na namba hizo bure bila malipo yoyote.
Na Neema Nandonde
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewataka wananchi kuendelea kutumia namba 3 muhimu, ambazo zinatumika katika kuzungumza na watoa huduma kwa wateja wa mitandao ya simu, kuripoti namba za matapeli na kuangalia usajili wa namba ambazo zimesajiliwa kupitia kitambulisho cha taifa (NIDA).
Akizungumza na redio Fadhila kwenye kipindi cha Asubuhi cha Morning Booster, April 10, 2025 kuhusu kampeni ya NI RAHISI SANA na SITAPELIKI Mhandisi wa TCRA Kanda ya Mashariki Khatibu Chande, amezitaja namba hizo kuwa ni namba 100, ambayo inatumika na mitandao yote ya simu kuwasiliana na wateja, hivyo wananchi wasidanganyike na namba za matapeli wanaojitambulisha kutoka kwenye mitandao ya simu.
Namba nyingine ni namba *106#, ambayo inatumika kuangalia namba ambazo zimesajiliwa kwa kutumia kitambulisho cha taifa (NIDA) cha mwananchi husika, hivyo atakapoona namba asizozifahamu zikiwa zimesajiliwa kupitia kitambulisho chake, akatoe taarifa mapema kwenye duka la mtandao wa simu husika.
Aidha namba ya tatu ni 15040 ambayo mwananchi atatumia kuripoti namba za mtu anayejihusisha na utapeli wa kimtandao, huku akisisitiza kuwa, mwananchi atatumia namba hizo bure bila malipo yoyote.
Sambamba na hayo, Mhandisi Khatibu amewasisitiza wananchi kuacha tabia ya kufungua viunganishi (links) hovyo, kutumie WIFI za bure ambazo huwajui wamiliki wake, kwani ni rahisi kwa wezi wa mtandaoni na wadukuzi kupata taarifa za mtumiaji wa mtandao.