TFS Kanda ya kusini yazindua kampeni ya upandaji wa Miti
27 January 2022, 12:25 PM
WAKALA wa huduma za misitu Tanzania (TFS) kanda ya kusini imezindua rasmi kampeni ya upandaji miti wilayani Masasi mkoani Mtwara katika kipindi hiki cha msimu wa mvua ambapo miti zaidi ya 50,000 inatarajiwa kupandwa katika maeneo mbalimbali ya wazi katika mji wa Masasi ikiwemo kwenye barabara zote za mji huo ofisi za serikali na taasisi binafsi na za umma.
Kampoeni hiyo imezinduliwa wilayani Masasi mkoani Mtwara ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo ya uzinduzi wa kampeni hiyo alikuwa ni mkuu wa wilaya ya Masasi, Claudia Kitta ambaye aliwaongoza viongozi mbalimbali wa serikali vyama vya siasa, watumishi wa serikali na wananchi wa mji huo.
Akizundua kampeni hiyo mkuu wa wilaya ya Masasi, Claudia Kitta amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa upandaji miti ikiwemo kupata kivuli pamoja na mji kuwa na muenekano mzuri.
Amesema kuwa faida zingine za upandaji miti no kupata matunda na mazao ya mbao ambayo pia yanaingiza fedha.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya ameitaka jamii kutunza mazingira pamoja na kuacha utamaduni wa ukataji misitu hovyo.
Wananchi mnatakiwa kufika katika ofisi za TFS kanda ya kusini zilizopo mji Masasi kwa kuchukua miche mbalimbali ya miti ili muweze kwenda kupanda kwenye maeneo yenu mbalimbali.