Wananchi Marika waishukuru serikali, mbunge Mwambe kwa kuwapatia maji safi na salama
5 November 2021, 4:06 AM
SERIKALI kupitia Wakala wa huduma za maji safi na usafi wa Mazingira vijijini( RUWASA) wilayani Masasi mkoani Mtwara, kwa mara ya kwanza tangu upatikanaji wa uhuru, 1961 imewapatia huduma ya maji safi na salama wananchi wa kitongoji cha Ipiho kilichopo kata ya Marika Halmashauri ya mji Masasi.
Jitihada za kuisukuma serikali kupeleka huduma hiyo ya maji kwa wananchi wa kata hiyo zimefanywa na Mbunge wa jimbo la Masasi, Geofyey Mwambe
Moja ya jitihada kubwa zilizofanywa na Mbunge Mwambe katika kuhakikisha wananchi wa kitongoji hicho wanaondokana na adha ya ukosefu wa maji ni kuwatafutia Pampu ya kusukuma maji ili kufungwa katika kisima ambacho kilichimbwa zaidi ya miaka 25 iliyopitwa lakini hakikutoa maji baada ya viongozi waliopo wilayani hapo kukitekeleza bila ya kujali kuwa fedha zilizotumika kuchimba kisima hicho ni za serikali.
Akizungumza na wananchi hao kijijini hapo leo (jana) katika zoezi la ufungaji wa Pampu hiyo na uzinduzi rasmi wa upatikanaji huduma hiyo ya maji, kwa niaba ya Mbunge , Mwambe , juma Pole amesema kuwa utekelezaji huo wa upatikanaji maji ni ahadi ya Mbunge baada ya kupokea kero kutoka kwa wananchi hao kipindi cha kampeni za uchaguzi pamoja na ziara zake za kuzunguza na wananchi wa jimbo lake hivi karibuni.
Katika kutimiza ahadi hiyo ya kuwapelekea huduma ya maji wananchi kitongoji hicho ambapo pia watanufaika na wananchi wa vitongoji vya jirani leo ofisi ya mbunge imeamua kuongozana moja kwa moja na kwenda kufunga Pampu hiyo na mafundi wa Ruwasa kuhakikisha wananchi hao wanapata huduma hiyo kama ilivyo ndoto za Mbunge Geoffrey mwambe.
Aidha, wananchi wa kitongoji hicho na kata ya Marika kwa ujumla wameipongeza serikali na Mbunge wa jimbo la Masasi , Mwambe kwa kuwapelekea huduma hiyo ya maji ambayo kwa miaka mingi wamekuwa hawaipati katika maeneo yao kwa uhakika.
Wamesema walikuwa wakinywa maji ya mabwawani kwa kushirikiana na wanyama huku maji hayo wakiyafuata umbali mrefu hadi kuyapata ambako kutokana na muda mwingi kuutumia kusaka maji hata shughuli zingine za kimaendeleo walizopaswa kuzifanya walikuwa hawazifanyi