CHAMA Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Kuweka Madawati Ya Lugha Ya Alama
19 May 2021, 5:38 AM
CHAMA Cha viziwi Tanzania (CHAVITA) tawi la mkoa Mtwara kimeiomba serikali kuweka madawati ya lugha ya alama katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Mtwara lengo likiwa ni kupunguza vikwazo vya mawasiliano kati ya viziwi na wahudumu wa afya.
Ombi hilo limetolewa mjini Newala na Mratibu wa Chama Cha viziwi Tanzania, mkoa wa Mtwara, Kassim Mchindula alipokuwa akiwamtambulisha mradi wa masuala ya afya na viziwi, mradi huo umefadhaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la The Foundation For civil Society ( FCS ) na kuratibiwa na CHAVITA Mtwara.
Mradi huo umetambulishwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Newala na kwamba utatekelezwa katika wilaya ya Newala pomoja na Tandahimba.
Mratibu huyo wa CHAVITA mkoani Mtwara, amesema kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano kwa viziwi pale wanapokwenda kupata matibabu kwenye vituo vya kutolewa huduma za afya wahudumu wa afya kutofahamu kutumia lugha ya alama ili kumuhudumia mtu mwenye ulemavu wa kutosikia.
Kupitia mradi huo CHAVITA Mtwara itatoa mafunzo ya lugha ya alama kwa wahudumu wa afya wa wilaya hizo ili wawe na ufahamu wa kutumia lugha hiyo na iwe rahisi kuwahudumia viziwi pale wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma hizo muhimu.