WANANCHI waishio vitongoji saba vilivyopo kata ya Nagaga wilayani Masasi wamechanga sh.5000
20 April 2021, 5:15 AM
WANANCHI waishio vitongoji saba vilivyopo kata ya Nagaga wilayani Masasi mkoani Mtwara wameamua kujitolea nguvu kazi kuchanga sh.5000 kwa kila kaya na kufyatua matofari lengo ni kujenga majengo mawili ya kisasa ambayo yatatumika kufunga vifaa tiba ikiwemo kiti cha kung’olea meno na mashine ya kufulia nguo kwenye kituo cha afya cha Nagaga.
Wananchi hao wameamua kujitolea kujenga majengo hayo kutokana na vifaa tiba hivyo wiki iliyopita kudaiwa kutaka kuhamishwa na uongozi wa halmashauri ya wilaya Masasi ili viende kufungwa katika hospitali ya halmashauri ya wilaya jambo ambalo wananchi hao walipinga vikali.
Kwa madai kuwa katika kituo cha afya cha Nagaga ambapo vifaa hivyo vipo kwa sasa hakuna majengo maalumu ya kuweka vifaa hiyo na kutoa huduma kwa wananchi.
Wakizungumza na waandishi wa habari wananchi hao wamesema kuwa watahakikisha wanajitoa kwa nguvu zote ili majengo hayo yakamilike kwa wakati ili kufunga vifaa hivyo hatimaye viweze kutoa huduma.
Aidha wananchi hao wa Nagaga wameeleza kuwa wataendelea kupinga kuhamishwa vifaa hivyo katika kituo chao na kwenda kufunga katika hospitali.
Vifaa hivyo vinaelezwa kukaa katika kituo hicho cha afya kwa miaka kadhaa bila kutumika kwa sababu ya kutokuwepo kwa majengo maalumu ya kufunga vifaa hivyo.
Hatua ambayo uongozi wa halmashauri iliwasukuma kutaka kuvihamisha na kutaka kwenda kuvifunga kwenye hospitali ya wilaya ambayo imejengwa katika kijiji cha Mbuyuni kata ya Mbuyuni na kuna majengo ya kuweka vifaa hivyo.