Micheweni FM

Shirikisho la walimu Zanzibar lampongeza Dkt. Mwinyi

1 July 2025, 9:59 pm

Makamo wa pili wa rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na shirikisho la walimu pamoja na wananchi katika ukumbi wa skuli ya Sekondari Utaani (picha na Ofisi ya makamo wa pili )

Katika kipindi cha miaka mitano, skuli mbali mbali zimejengwa za kisasa zikiwa na majitaji yote ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo maabara za kisasa za masomo ya sayansi, maktaba, vyoo, vyumba vya kompyuta, sambamba na kufanyika kwa mgao wa vitabu vya kusomea na kufundishia zaidi ya milioni tatu kwa skuli zote.

Na Mwiaba Kombo

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA) imetekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa wa kupigiwa mfano.

Hemed ameyasema hayo kwenye ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Shirikisho la Walimu Zanzibar, kwa ajili ya kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, lililofanyika katika ukumbi wa skuli ya Utaani iliyopo Wete  Mkoa wa Kaskazini Pemba

Amesema katika kipindi cha miaka mitano, wizara ya elimu imesimamia vyema miundombinu ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, ambapo jumla ya skuli 36 za ghora kwa ngazi ya msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar zimejengwa.

Kwa upande wake, waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa, amesema Shirikisho la Walimu linaishukuru serikali ya awamu ya nane kwa kuipa hadhi sekta ya elimu, kuimarisha miundombinu ya elimu sambamba na kuwaangalia kwa karibu walimu na watendaji wa wizara ya Elimu.

Akisoma risala ya Shirikosho la Walimu Zanzibar, Khamis Othman amesema lengo la kongamano hilo ni kurejesha shukurani kwa Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Mwinyi kwa hadhi waliyoipandisha kwa sekta ya elimu na walimu pamoja na kuimarishwa kwa mazingira ya kusomea na kufundishia, kuondolewa ada kwa wanafunzi ambapo wanasoma bila ya malipo.