Wahitimu wa JKT wahimizwa kuwa na matumizi sahihi ya mitandao
May 7, 2024, 6:45 am
Na Denis Sinkonde,Songwe
Mkuu wa Ukaguzi JWTZ, Meja Jenerali Kahema Mzirai amewaasa wahitimu wa mafunzo ya awali ya JKT Kikosi cha Itaka kufanya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kuepuka mazara ya mitandao hiyo
Ametoa rai hiyo leo Jumatatu Mei 6, 2024 wakati akifunga rasmi mafunzo ya ya awali katika Kikosi 845 KJ Itaka wilayani Mbozi mkoani Songwe
Meja Jenerali Mzirai amesema kuwa anawasa na kuwakumbusha juu ya matumizi bora ya mitandao ya kijamii kutokana na kukua kwa teknolojia.
“Kutokana na utandawazi kila mtanzania anatamani kutumia simu janja ambazo zimekuwa na mambo mengi sana ambapo Kila mtu anatamani kujua nini kinachoendelea duniani
Lakini baadhi ya vijana wamekuwa hawana elimu ya kutosha juu ya matumizi sahihi ya mitandao hiyo, hivyo kutazama mambo ambayo ni kinyume kabisa na maadili na tamaduni za kiafrika” amesema na kuongeza;
“Natumia fursa hii kuwaasa, hatukatai kutumia mitandao hii ila ni vyema mkatumia kujipatia elimu ya mambo mema ambayo yatawasaidia katika maisha yenu binafsi na taifa kwa ujumla
Sote tunajua serikali imetunga sheria kudhibiti maudhui ya mtandaoni ambapo utakapo tumia au kuonyesha jambo ambalo ni kinyume na desturi zetu hatua Kali zitachukuliwa dhidi yako. Hivyo tuwe makini sana katika matumizi ya mitandao” amesisitiza