Micheweni FM
Micheweni FM
30 September 2025, 8:01 am

Viongozi wa soko la Tumbe wametakiwa kusimamia kwa umakini suala la usafi katika soko hilo ili liwe na haiba nzuri na mvuto kwa wageni wanaotembelea eneo hilo.
Na Mwiaba Kombo
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Khatibu Juma Mjaja, wakati akizungumza na wananchi pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, mara baada ya kumaliza zoezi la usafi lililofanyika katika soko hilo.
Amesema kuwa ili soko hilo pamoja na maeneo ya jirani yaweze kubaki katika hali nzuri, ni lazima viongozi wa soko wasimamie ipasavyo shughuli zote za usafi na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote.
Sauti ya mkuu wa wilaya Khatib Juma Mjaja akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Hamad Khatib Saleh, amewataka wananchi wa kijiji cha Tumbe kuendelea kushirikiana na halmashauri katika kuhakikisha suala la usafi linapewa kipaumbele.
Nao wananchi wa eneo hilo wameishukuru halmashauri kwa kuendelea kuendesha shughuli za usafi katika maeneo yao, wakisisitiza kuwa usafi ni jambo muhimu katika ustawi wa jamii na afya zao.
Siku ya Usafi Duniani huadhimishwa kila ifikapo Septemba 20 ya kila mwaka, ambapo katika Wilaya ya Micheweni maadhimisho hayo yamefanyika kwa kufanya usafi katika soko la samaki na mboga mboga la Tumbe.