Ng’ombe 153 wakabidhiwa kwa vikundi vya ushirika Pemba
2 September 2024, 1:40 pm
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa ng’ombe 153 wa kufugwa kisiwani Pemba ambayo itakuwa ni chachu ya kuwaletea maendeleo wananchi hao.
Na Mwiaba Kombo
Waziri wa kilimo, Umwagiliaji, Mifugo na Maliasili Zanzibar Shamata Shaame Khamis amewataka wafugaji hao kuhakikisha wanafuata maelekezo kutoka kwa wataalam wa mifugo ili waweze kufuga ng’ombe hao kwa utaalam mzuri ambao utaondosha maradhi kwa ng’ombe.
Ameyasema hayo wakati akikabidhi ng’ombe wa maziwa kwa vyama vya ushirika katika shehia ya Kiungoni wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ambao wametolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa kushirikiana na mradi wa TI3P na shirika la Heifer International Tanzania.
Aidha Shamata ametoa rai kwa wafugaji wa ng’ombe hao kuhakikisha wanafuga kwa tija ili kujiletea maendeleo ambayo yataweza kujikwamua na hali ya maisha .
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib amessema dhamira ya serikali ni kuleta maendeleo na kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na maendeleo hayo.
Mkuu huyo wa mkoa amewataka wafugaji hao kuhakikisha wanawatunza ng’ombe hao ili waweze kuzaliana na kuweza kupata faida ambazo zitawaletea tija.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Mifugo na Maliasili Ali Khamis Juma amewataka wakuu wa idara kuhakikisha wanakuwa karibu na wafugaji hao ili kuweza kutatua changamoto ndogondogo katika ufugaji wao.
Kwa upande wake mjumbe kutoka TADB Dammas Damian amesema zaidi ya million mia nane na themanini na saba za kitanzania zimetumika kununulia ng’ombe hao ambao wanatoka Afrika Kusini.
Amewataka wafugaji hao kuhakiksha wanaleta mageuzi katika jamii baada ya kupata ng’ombe hao na kuhakikisha wanainua vipato vyao .
Zaidi ya ng’ombe 153 wametolewa kisiwani Pemba ambapo mkoa wa Kaskazini Pemba wamepata 137 na Kusini Pemba 16 mbapo kikundi cha jitihada kutoka Kifundi kimepata 16, Tundwa kutoka Piki 16, Zinamola kutoka Kinyasini 16, Tumeridhika kutoka Finya 16 , Tuko Imara kutoka Kiuyu 30, Kiuyu 14 na Kinyasini Kaminishe ni 17.