Zaidi ya wanafunzi 200 wasoma chini ya mti skuli ya Minungwini
29 March 2024, 9:36 am
Skuli ya Minungwini ni baadhi ya skuli ambayo ipo katika wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba na ni miongoni mwa skuli ambazo zimejengwa kwa muda mrefu na miundombinu yake imechakaa.
Na Zuhura Juma
Wanafunzi 274 wa skuli ya msingi Minungwini wilaya ya Wete Pemba, wanaendelea kusoma chini ya miti baada ya vyumba vinne vya madarasa walivyokuwa wakitumia kuchimbuka na kuvuja kwa muda wa zaidi ya miezi sita sasa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wazazi na walezi wenye watoto skulini hapo wamesema, wanafunzi hao wanaendelea kukosa mtiririko mzuri wa masomo kutokana na kutumia eneo hilo kwa siku za kiangazi pekee huku siku za mvua zikiwa ni changamoto.
Wazazi hao wamesema kuwa, kutokana na kuharibika kwa madarasa hayo wana hofu ya kuporomoka kwa elimu skulini hapo kutokana na changamoto ya wanafunzi hao kusoma chini ya miti.
Mmoja kati ya wazazi hao Fatma Jaffar Faki alisema kuwa hali hiyo haimpi usingizi kutokana na watoto wao kutokuwa na mazingira rafiki ya kusomea.
Mzazi Asha Omar Rashid ameiomba Wizara ya elimu kuchukua hatua za haraka kujenga ili kuwarejesha wanafunzi madarasani.
Akizungumzia kuwepo kwa vyumba hivyo chakavu alisema, vinaweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi, walimu na wapita njia.
Mwalimu Mkuu skuli hiyo Ahmada Ali Omar amesema, ubovu wa banda hilo umesababisha wanafunzi 274 kukosa sehemu ya kukaa na badala yake wanawaweka chini ya miti, ili kuhakikisha na wao wanapata elimu kama kawaida.
Mwalimu huyo anawashukuru sana viongozi wao wa Serikali, majimbo na shehia kwa ushirikiano wanaouonesha katika kuhakikisha wanapeleka maendeleo ya elimu mbele.
Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim amesema kuwa, changamoto hiyo wameiona ambapo wana mpango wa kujenga skuli ya ghorofa pamoja na kuyafanyia ukarabati madarasa chakavu, ili kuondosha tatizo hilo.
Aidha ameipongeza skuli hiyo kwa kutoa ufaulu mzuri kwa wanafunzi wao, ambapo umetokana na ushirikiano mzuri kati ya wazazi, kamati ya skuli, walimu na Serikali kupitia Wizara na kuwataka kuendeleza mashirikiano, ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
Skuli ya msingi Minungwini ina wanafunzi 2,277 na walimu 42, ambapo wanakwenda mikondo miwili asubuhi na mchana.