Waziri Soud aona mbali sekta ya viungo Tanzania
9 December 2021, 10:55 am
NA ZUHURA JUMA,
WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Soud Hassan Nahoda amesema, Tanzania ina nafasi kubwa ya kuendeleza sekta ya viungo ili kupanua wigo wa kufikia ubora wa soko la bidhaa hizo.
Akizungumza katika Kongamano la kusaidia minyoyoro ya thamani kwa ajili ya Ustawi wa pamoja (Agri-connect) lililofanyika katika Ikumbi wa hoteli ya Misali Wesha Chake Chake alisema, kuna viungo zaidi ya 30 vinavyostawi vizuri visiwani hapa, hivyo ipo haja ya kuchangamkia fursa hiyo inatayowapatia tija wakulima na Taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa, madhumuni ya mradi huo ni kusimamia maendeleo ya sekta binafsi kuongeza tija na uhakika wa chakula kupitia ongezeko la tija la biashara na ushindani kwenye kilimo cha kahawa Kusini mwa Tanzania Bara na milimo cha mboga, matunda na viungo kwa visiwa vya Zanzibar.
“Twende na Kilimo hai ambacho kina thamani kubwa, kwani tutapata fedha nyingi na tija kwa wakulima wetu na Taifa kwa ujumla, naamini katika Kongamano hili tutajadili na kubaini suluhisho pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwenye biashara ya viungo”, alisema Waziri huyo.
Aidha ameeleza kuwa, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar aliushukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa mchango wao mkubwa kupitia mradi huo unaolenga wahusika wote wa mnyororo wa thamni kwa mazao ya kahawa, chai, mboga, matunda na viungo.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Pemba Hakimu Vuai Shein alisema, jitihada zinahitajika kusimamia uzalishaji wa bidhaa zenye ubora, ili kuendana na soko la nje.
Akitoa maelezo katika Kongamano hilo, Kiongozi wa timu ya mradi wa Agri-connect Colin Scott alisema, mradi huo utaboresha maisha ya wakulima wadogo 150,000 katika nyanda za juu Kusini mwa Tanzania na Zanzibar, ambao utachangia katika ukuaji shirikishi wa uchumi, maendeleo na uwekezaji katika sekta binafsi, utengenezaji wa ajira na kuboreshwa kwa usalama wa chakula na lishe.
Aidha ameeleza kuwa, mradi huo unazingatia kuongeza mnyororo wa thamani kwa kuboresha uzalishaji, isindikaji na uuzaji, kusaidia uboreshaji wa sera zinazojenga mazingira wezeshi na uwekezaji wa sekta binafsi, kuwaunganisha wakulima na masoko kupitia uwekezaji katika ukarabti wa barabara vijijini.
Nae Mkuu wa Wilaya Chake Chake, Rashid Abdalla Rashid aliipongeza Wizara ya kilimo kwa kuona umuhimu wa kuendeleza kilimo hicho, sambamba na kuushukuru Umoja wa Ulaya kwa kuisaidia kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia shughuli mbali mbali ikiwemo sekta ya Kilimo.
Mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na EU ambao unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wakulima 150,000 kwa Tanzania Bara na visiwa vya Unguja na Pemba.