MWANASHERIA: Wazazi, Walimu, musiwe miongoni mwa wanaodhalilisha watoto
6 December 2021, 11:03 am
Na Mwiaba Kombo
WAZAZI na walimu wameshauriwa kuwalinda watoto dhidi ya udhalilishaji na kuepuka kuwa miongoni mwa watendaji wa matendo hayo.
Akizungumza na wanafunzi katika skuli ya Maandalizi Madungu Chake Chake, mwanasheria kutoka Kituo cha Huduma za Sheria (ZLSC) Pemba Siti Habib Mohamed alisema, ipo haja ya kuwasaidia watoto wasifanyiwe udhalilishaji wanapokuwa skuli, madrasa na nyumbani.
Amesema kuwa, ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha watoto wanakuwa salama muda wote, huku wazazi na walimu wakiepuka kuwafanyia watoto hao udhalilishaji, kwani inaaminika kwamba wanakuwa kwenye mikono salama.
Ameishauri jamii kwa ujumla waendelee kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbali mbali katika kupambana na janga hilo, ili kumlinda mtoto na kuhakikisha anapatiwa zile haki zote za msingi.
Kwa upande wao wanafunzi walipokuwa wakiulizwa athari za udhalilishaji walijibu kuwa, inaweza kusababishia mtoto maradhi, kifo, kuathirika kimwili, kisaikolojia na hata kuweza kukosa elimu na kupelekea kushindwa kutimiza ndoto zake za baadae.
Nao walimu wa skuli hiyo wamekishukuru kituo hicho kwa kuona umuhimu wa kuwapa elimu wanafunzi wao, wanaamini itazidi kuwasaidia kujikinga na kuripoti pale wanapofikwa na majanga hayo.
Mkutano huo ulifanyika katika skuli ya Madungu Chake Chake ambao umeandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Pemba ikiwa wanaadhimisha siku 16 za kupinga ukatili na Udhalilishaji kwa wanawake na watoto.