Waandishi acheni woga ibuweni habari za rushwa(Zaeca)
12 November 2021, 5:58 am
Na Mwiaba Kombo
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar ‘ZAECA’ ACP, Ahmed Khamis Makarani, amewataka waandishi kuacha woga na kuandika habari za wala rushwa na watoaji, kwani hiyo ndio sehemu ya uwajibikaji.
Amesema, uwajibikaji wa kweli na wenye nia ya kujenga, haiwezekani kukosa kulaaniwa, kusemwa, kutengwa na kuonekana tofauati ndani ya jamii.
ACP Makarani, ameyasema hayo ukumbi wa Wizara ya fedha Gombani Chake chake Pemba, wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya kuelekea maadhimisho ya kupinga rushwa duniani Disemba 9, mwaka huu.
Aidha amesema sauti ya waandishi wa habari, jinsi inavyofika mbali kwa muda mfupi, iwapo wataacha woga na kujihariri wenyewe, wanaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa, mapambano dhidi ya rushwa.
Amewataka waandishi, kuendelea kuitumia ofisi ya ZAECA Pemba, kwa ajili ya kujua kazi, changamoto na mafanikio yanayopatikana katika mapambano dhidi ya rushwa.
Akiwasilisha mada, ya wajibu wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa, mtoa mada Ali Mbarouk Omar, amesema waandishi wa habari wanayo nafasi wa kuyaibua yale matatizo ambayo yanaashiria viashiria vya rushwa katika jamii.
Nae Mratibu wa TAMWA-Pemba Fat-hya Mussa Said, amesema wanawake wamekuwa wahanga wakubwa wa kuombwa rushwa hata ya ngono, wakati wanapotaka kugombea.
“Baadhi ya wanaume, wamekuwa wakivunja haki za wanawake na hasa kwenye uongozi, maana wamekuwa wakitakiwa kutoa rushwa tena sio ya fedha kwa sasa, ni ya ngono,’’alilalamika.
Hata hivyo amesema pamoja na changamoto hiyo, amesema kunaongezeko la wanawake kuomba nafasi mbali mbali majimboni kwa mwaka 2020, ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2015.
Baadhi ya waandishi wa habari, waliiomba ofisi ya ZAECA Pemba, kuendelea kuwa karibu na waandishi wa habari, ili kupata habari kadhaa wanazoziibua watendaji wao.
Mwandishi Ali Massoud Kombo kutoka Jamii tv, amesema wakati umefika maafisa wa vituo vya ‘ZAECA’ kujibu hoja za waandishi hasa kwa matukio, yaliotokea kwenye maeneo yao.
Mwandishi Kheir Juma Basha, amesema elimu ya sheria ya ‘ZAECA’ bado inahitajika kwa jamii, ili wajue wajibu na nafasi yao wanapobaini uwepo wa rushwa katika tasisi.
Mafunzo hayo yameandaliwa na ZAECA kwa ushirikiano na TAMWA, na ni sehemu ya kuelekea kilele cha maadhimisho siku ya kupinga rushwa duniani, ambayo huadhimishwa kila ifikapo Disemba 9 ya kila mwaka na ujumbe wa mwaka huu ‘ni haki yangu, wajibu kukataa rushwa’.